Saturday, November 17, 2007

Uingereza yapunguza gharama za viza









UBALOZI wa Uingereza nchini, umepunguza viwango vya gharama za kuomba viza kwa wasafiri wanaotaka kwenda nchini mwao kutokana na kuimarika kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania. Ofisa Habari wa Ubalozi wa Uingereza John Bradshaw aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu, Ubalozi huo umepunguza gharama za viza zote baada ya kuona Shilingi ya Tanzania imeimarika kiwango cha juu. Bradshaw alizitaja gharama zilizoshuka kuwa ni za viza za matembezi ya miezi sita kuwa ni Sh 157,000 (zamani Sh 176,000), viza ya matembezi ya muda mrefu Sh 500,000 (zamani Sh 560,000), viza kwa ajili ya matibabu Sh 157,000 (zamani Sh 176,000), viza ya wanafunzi Sh 225,000 (zamani Sh 277,000), viza ya kupitia Sh 110,000 (zamani Sh 123,000) na ya makazi na ndoa Sh milioni 1.25 (zamani Sh milioni 1.4). Thamani ya Shilingi imezidi kuimarika dhidi ya sarafu nyingine muhimu za dunia kama vile Dola ya Marekani, Euro na Pauni ya Uingereza. Hadi jana Dola ilikuwa ikinunuliwa kwa Sh 1,000, Pauni Sh 2,355 na Euro Sh 1,645, tofauti na hali ilivyokuwa miezi minne iliyopita. Ofisa huyo ubalozi pia aliwataka wanaotaka kuomba viza katika msimu huu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kupeleka maombi yao mwezi mmoja kabla washughulikiwe bila usumbufu kwa sababu wakati wa sikukuu wafanyakazi wengi wa ubalozi huo wanakwenda likizo. Alisema ili kurahisisha maombi ya viza wameanzisha utaratibu maalumu wa kujaza fomu za maombi bila kufanyiwa usaili wa uso kwa uso kwa sababu maswali yote yamewekwa kwenye fomu hizo. “Nawashauri waombaji wawahi kutuma maombi yao, tena ni vizuri wakijaza fomu hizo kupitia mtandao ambao unarahisisha na kupunguza foleni,” alisema Bradshaw. Bradshaw alisema kuwa katika uchunguzi uliofanywa Aprili mwaka huu, kati ya maombi 144, waombaji 32 sawa na asilimia 22 walipeleka vielelezo bandia. Alisema watu kati ya 50 na 60 huomba viza kila siku Ubalozini hapo na zaidi ya asilimia 80 ya waombaji hupata viza.

Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu