|
---|
Habari za Kitaifa | | Tume yamtangaza Kibaki | NAIROBI, Kenya HabariLeo; Sunday,December 30, 2007 @20:01
| RAIS Mwai Kibaki jana alitangazwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Alhamisi iliyopita, uliokuwa wa ushindani mkubwa katika historia ya nchi hiyo na uliogubikwa na tuhuma za wizi wa kura na siku mbili za machafuko baada ya matokeo kuchelewa kutangazwa.
Muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi majira ya saa 11:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, Kibaki (76) aliapishwa kwenye Ikulu ya Nairobi saa moja baadaye, kuliongoza Taifa hilo kubwa kiuchumi la Afrika Mashariki kwa muhula wa pili na wa mwisho. Kibaki aliyegombea kwa tiketi ya chama cha PNU, ameshinda tena kiti hicho kwa kumwangusha mpinzani wake mkuu, Raila Odinga wa Orange Democratic Movement (ODM).
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK), Samwel Kivuitu, alimtangaza Kibaki mshindi kwa kupata kura 4,584,721 na Odinga kura 4,352,993 huku mgombea kwa tiketi ya ODM-Kenya, Kalonzo Musyoka akipata kura 877,992. Kibaki amemshinda Odinga kwa tofauti ya kura 231,728. “Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Mwai Kibaki ndiye mshindi,” alisema Kivuitu, ambaye awali alikuwa akiheshimiwa sana kwa kuongoza vyema Uchaguzi Mkuu wa 2002.
Kwa matokeo hayo yaliyotangazwa moja kwa moja kupitia Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) pekee baada ya waandishi wengine wa habari, wa ndani na nje ya nchi hiyo, kuondolewa ndani ya ukumbi huo baada ya mwenyekiti huyo wa ECK kulazimika kuondolewa ndani ya Ukumbi wa Kimataifa wa Kenyatta, kwa nguvu za askari wa kutuliza ghasia (GSU). Akizungumza baada ya kazi hiyo ya kuapishwa iliyosimamiwa na Jaji Mkuu wa Kenya, Evan Gicheru, Rais Kibaki aliwataka wanasiasa wenzake kuungana naye pamoja kuijenga Kenya.
Hata hivyo, licha ya kauli yake hiyo tayari machafuko yameripotiwa katika baadhi ya maeneo baada ya matokeo hayo kutangazwa. Maeneo hayo ni ngome ya Odinga, mjini Kisumu, ambako watu walikataa matokeo na kufanya vurugu wakidai kumekuwapo wizi wa kura; Mombasa vijana walifanya fujo mtaani kwa kuchoma matairi, hali iliyowafanya polisi kufyatua risasi na mabomu ya machozi.
Wakati Kibaki anaongoza kura za urais na kutangazwa kushinda, chama chake cha PNU kimepata viti 33 vya ubunge huku ODM ikiongoza kwa viti vingi, 95, na chama cha Kalonzo kushinda viti 10 vya ubunge.
Matokeo hayo yaliyotangazwa katika Ukumbi wa Kimataifa wa Kenyatta, yalichelewa kutolewa kwa siku mbili kutokana na baadhi ya matokeo ya majimbo kuchelewa. Hali hiyo ilisababisha kuwapo kwa hisia kuwa kura ziliibwa hasa ikizingatiwa kuwa viti vingi vya ubunge vimechukuliwa na ODM.
ECK ililazimika kuahirisha kutoa matokeo kutokana na vurugu zilizotawala katika chumba cha mkutano ambacho mawakala wa vyama vya siasa waliokuwapo pamoja na waandishi wa habari walifanya vurugu na fujo.
Vurugu hizo zilitokea wakati Mwenyekiti wa ECK, Kivuitu alipoanza kutoa matokeo ndipo alipoinuka mtu mmoja na kupiga kelele za ‘Haki, hii sio Nchi ya Polisi’, hali iliyomfanya kusitisha na polisi kumsindikiza kutoka nje ya ukumbi. Muda mfupi baada ya Kivuitu kulazimishwa kutoa matokeo yote, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ODM, Odinga, alichukua kipaza sauti.
“Hapa kinachofanyika ni uchezeaji wa kura,” aliwaambia mamia ya waandishi wa habari na mawakala wa vyama vya siasa waliokuwapo kwenye chumba cha kutangaza matokeo wakizungukwa na wanajeshi. Awali kulikuwa na fujo na watu wakipiga kelele, hali iliyomfanya Kivuitu kutaka utulivu ili aweze kutoa matokeo, lakini ilishindikana na kumfanya atoke nje ya ukumbi.
Mapema jana mchana, Odinga ambaye amekuwa ‘mpikaji wa siasa za Kenya’ kwa muda mrefu, aliituhumu serikali kwa kupanga kuiba kura baada ya yeye kuongoza tangu baada ya kuanza kuhesabu kura. Alitaka kuhesabiwa upya kwa kura mjini Nairobi huku wakiwapo waangalizi na waandishi wa habari. Alimtaka Kibaki kukubali kushindwa ili amwachie mwenzake asukume mbele demokrasia.
“Tumeitaka ECK kuagiza kuhesabiwa upya kwa kura kwa Nairobi. Ikiwa Kibaki atatangazwa kuwa mshindi, matokeo yake yatakuwa makubwa kuyadhibiti, hatutaki kuipeleka Kenya kama Ivory Coast. “Namuomba Kivuitu kujiuzulu kuliko kutangaza matokeo ya wizi kwa nchi yake,” mwanasiasa huyo tajiri aliyewahi kufungwa jela, aliwaambia waandishi wa habari.
Tangu uchaguzi wa Kenya ufanyike Desemba 27, mwaka huu, kumekuwa na vurugu zikitokea sehemu mbalimbali na kusababisha watu 14 kupoteza maisha na nyumba na maduka kuchomwa moto hasa katika maeneo ya Kibera na Mathare katika Jiji la Nairobi. | | | | |
|
---|
|
---|
| Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved |
|
---|
|
|