Tuesday, April 14, 2009

DECI katika mauti!

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema shughuli za Kampuni ya DECI
(Development Enterprenueurship Community Initiative) za wanachama
kuweka fedha kupata faida marudufu ni sawa na upatu na ni kinyume cha
sheria za nchi.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake jijini Dar
es Salaam leo (Jumanne Apr. 14, 2009) alisema ndiyo maana Serikali
imeunda timu ya kuingalia DECI na kuchukua hatua bila kuwaathiri
wanachama wa DECI.
“Hakuna cha maono wala ufunuo, DECI ni upatu tu. DECI siyo mkombozi ni
ujanja ujanja ambao ambao lazima utaleta matatizo hatimaye,” alisema.

Shughuli za upatu ni kinyume cha sheria Na. 8 ya mwaka 2006,
iliyoidhinishwa na Rais Januari 5, mwaka 2007, kuwa ni kosa kuendesha
shughuli za upatu ambao hauna usalama wa fedha za watu wanazochanga,
aliongeza.

Alisema kuwa timu iliyoundwa na serikali kuangalia shughuli za DECI
ina wataalamu kutoka Benki Kuu, Wakala wa Soko la Mitaji na Dhamana
(Capital Markets Authority) na Idara ya Polisi.


DECI ilianza shughuli zake nchini mwaka 2007 na iliandikishwa kwa
Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA).


Waziri Mkuu alisema DECI ilianzishwa kama chama cha kuweka na kukopa,
lakini baadaye ikawa inaendesha upatu na kwamba ina wanachama zaidi ya
430,000 na ina ofisi 46 katika mikoa 18 kati ya 26 nchini, kwa mujibu
wa taarifa alizonazo.

Benki ina akiba ya Sh. bilioni 1, lakini fedha ambazo zimezungushwa
kupitia DECI ni Sh. bilioni 13 ambazo zilitolewa na kuchukuliwa na
wanachama kama faida.

Kuhusu suala la ardhi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri Mkuu
alisema kuwa suala la ardhi linatawaliwa na sheria za kila nchi na
siyo la ushirikiano katika jumuiya.

Alisema suala ardhi, kama vile la hoja ya mtu akiikaa katika nchi moja
kwa mfululizo kwa miaka mitano apate uraia wa nchi hiyo, ni masuala
ambayo hayawezi yakachukuliwa kwa pupa na Tanzania lazima iyaangalie
kwa makini.

Kuhusu udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma ambavyo baadhi yao
vilifungwa kwa muda kutokana na suala la uchangiaji, Waziri Mkuu
alisema udahili umekwenda vizuri na kunavigezo vipya vya kujua uwezo
wa mwanafunzo kucjangia kiasi gani.

Waziri Mkuu pia alisema Tanzania isisite kuhusu kuwaruhusu wakulima
wakubwa binafsi kuwekeza katika kilimo cha kisasa cha kibiashara kwani
bado kuna ardhi kubwa yenye rutuba lakini haijaguswa.

Alisema kinachotakiwa ni kuwa na Benki ya Ardhi ili muwekezaji akitaka
kuwekeza katika kilimo anapewa ardhi ambayo kwa mfumo wa Tanzania ni
ya Serikali na inatolewa kwa kukodishwa kwa masharti maalum.

Kuhusu uvunjifu wa amani huko Tarime na maeneo mengine katika mkoa wa
Mara, Waziri Mkuu alisema Serikali imepanga kuwa na mkoa wa kipolisi
wilayani Tarime ili kuimarisha ulinzi.

Vilevile, inafaa kutenga eneo la amani la watu kuweza kukimbilia kama
vile kuwa na kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika maeneo yenye
magomvi.

Kuhusu maagizo ya Waziri Mkuu kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) kuangalia hesabu za Kituo cha Mabasi cha Ubungo na
Soko la Kariakoo, Waziri Mkuu alisema kazi hiyo imekwishaanza na
kwamba amepewa muda wa kutosha kuikamilisha.

(mwisho)

Imetolewa na:

Ofisi ya Waziri Mkuu

S.L.P. 3021

DAR ES SALAAM

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu