Wana habari wa pwani kufanya maandamano ya amani
Na John Gagarini, Kibaha RAIS wa Chama cha Waandishi wa Habari Nchini (UTPC) Bw Keneth Simbaya kesho anatarajiwa kuwa wa mgeni rasmi kwenye maandamano ya amani yatakayofanywa na klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Pwani (CRPC) kupinga mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Chanel Ten mkoani Iringa Bw Daud Mwangosi. Hayo yalisemwa jana na mwenyekiti wa chama cha waandishi wa Habari mkoani Pwani CRPC Bw Masau Bwire alipoonge na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha na kusema kuwa maandamano hayo ambayo yalikuwa yafanyike jana yalishindwa kufanyika baada ya Jeshi la Polisi mkoani Pwani kusema kuwa walikiuka taratibu za maandamano. Bw Bwire alisema kuwa Jeshi la polisi waliwazuia kwa madai kuwa taratibu za maandamano kisheria zinataka mwombaji aombe muda wa saa 48 ambapo wao waliomba jana hivyo kushindwa kukidhi vigezo hivyo vya kisheria. “Tuliamua kutii sheria kwa kuhairisha maandamano hayo licha ya kuwa wenzetu mikoani walifanya jana na sisi kesho tutafanya hivyo waandishi wasiwe na wasiwasi, na tunatarajia mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni Rais wa UTPC Bw Simbaya hivyo tunaamini maandamano hayo yatakuwa na nguvu yaiana yake,” alisema Bw Bwire. Alisema lengo la maandamano hayo ni kuungana na waandishi kote nchini kupinga mauaji hayo yaliyofanywa na polisi jambo ambalo limeleta mtafaruku mkubwa baina ya waandishi na jeshi hilo. “Kwa kweli inasikitisha kuona mwenzetu akiuwawa kwenye masuala ya kisiasa akiwa anatekeleza majukumu yake ya kuuhabarisha umma nini kinachoendelea,” alisema Bw Bwire. Mwenyekiti huyo wa CRPC alisema kuwa maandamano hayo yatapita kwenye maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na barabara kuu ya Morogoro, barabara ya ofisi ya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, sokoni, stendi, sheli na kuishia viwanja vya mpira wa miguu vya Bwawani Maili Moja wilayani Kibaha. Aliwataka waandishi wa habari kujitokeza kwa wingi kwenye maandamano hayo ili kuonyesha umoja wao na kutetea maslahi yao na kuungana na familia ya marehemu katika kumuenzi. Aidha alisema kuwa katika maandamano hayo mgeni rasmi atatoa tamko la UTPC na CRPC nayo itatoa tamko la mkoa wa Pwani. Mwisho.