Amina Chifupa: Wazazi wake wajaa hou
Kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalimu kupitia Umoja wa Vijana wa CCM, marehemu Amina Chifupa, kimezidi kuzua mapya huku kikileta hofu kubwa katika familia yake. Baba mzazi wa marehemu Amina, Luteni Mstaafu Hamis Gabriel Chifupa, amesema anahofia usalama wa familia yake iwapo atatangaza majina ya watu aliotajiwa na mwanae kabla ya kifo chake kwamba wanahusika kwa njia moja ama nyingine na maradhi yake. ``Kabla hajafa alikuwa akitaja majina ya baadhi ya viongozi, wengine ninyi waandishi mmekwishawataja, lakini wengine bado, pamoja na hayo mimi siwezi kuwataja kwa kuhofia usalama wangu na familia yangu, naiachia Serikali ifanye kazi hiyo,`` akasema Mzee Chifupa. Akasema mwanae aliugua maradhi ya ajabu ambapo alikuwa akitaja majina ya baadhi ya viongozi kuwa ndio waliomsababishia tatizo la kuugua. Akasema katika kipindi hicho chote Amina alikuwa hali chakula chochote na ndipo walipobaini kuwa yalikuwa mambo ya kiswahili, hivyo ikabidi kumuhudumia kiswahili. Hata hivyo huduma hizo za kiswahili hazikufua dafu na ndipo walipoamua kumpeleka katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo. Mzee Chifupa akasema akiwa hospitalini Amina aliendelea kutamka maneno mengi mazito na ya ajabu yaliyoashiria kifo chake. ``Familia haiwezi kusema Serikali ichunguze, ila kama kuna mtu mwenye taarifa au anayejua mazingira ya kifo cha mwanangu anaweza kutoa taarifa serikalini ili wanaohusika wachukuliwe hatua,`` akasema. Amina Chifupa alifariki dunia Juni 26 mwaka huu katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Tuma Maoni Yako