Zaidi ya watu Milioni. 1.6 waripotiwa kubugia bangi 2007-07-13 17:19:52 Na Jacqueline Mosha, Jijini
Zaidi ya watu Milioni 1.6 wameripotiwa kutumia bangi duniani kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2003 mpaka 2005 ambapo umri unaoathirika zaidi umetajwa kuwa ni kuanzia miaka 15 mpaka 64. Akiongea na Alasiri, Ofisa katika Tume ya kuratibu udhibiti wa dawa za kulevya nchini, Bw. January Ntisi amesema kiwango hicho kinatokana na ripoti ya dunia ya madawa ya kulevya iliyotolewa mwaka 2006. Ofisa huyo amesema vijana wengi wameshaathirika sana na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi. Amesema Tume hiyo inajitahidi kwa hali yoyote ile ili kusaidia kuwaondoa mtegoni walioanza kutumia dawa hizo na kuepusha watumiaji wapya kuongezeka. ``Vijana wengi wanaotumia dawa hizi huwa ni vigumu sana kwao kuacha kabisa kutumia kwakuwa kati ya asilimia 100 ya watumiaji waliokwisha athirika na dawa hizo, basi asilimia 5 tu ndio labda wanaweza kuacha kabisa kutumia baada ya kupatiwa tiba toka hospitalini na kupewa ushauri nasaha,`` akasisitiza. Lakini Bw. Ntisi anasema idadi hiyo ya asilimia 5 kwa wanaokisiwa kuweza kuachana na matumizi ya dawa hizo ni ndogo sana ukilinganisha na asilimia 100 ya watumiaji wote, hivyo juhudi za dhati zinatakiwa kufanywa kwa kushirikisha jamii na Tume hiyo ili kuepusha janga lisizidi. ``Tatizo linalochangia kuongezeka kwa matumizi haya ni kwamba mtu aliyezowea kutumia dawa za kulevya hushindwa kuishi bila ya kuzitumia�anapokuwa arosto, atatumia njia yoyote ikiwemo wizi, uporaji na hata ukabaji na vitendo vingine vya kihuni ili tu apate pesa kidogo ya kununulia dawa hizo ili ajitibu,`` akabainisha Bw. Ntisi. Aidha Bw. Ntisi amesema jumla hiyo ya watu 162,400,000 ni sawa na asilimia 3.9 ya watumiaji wote wa bangi duniani ambapo kuanzia mwaka 2003 mpaka 2005, takwimu zilionyesha kuwa bara la Ulaya kulikuwa na idadi ya watumiaji bangi 30,800,000 sawa na asilimia 5.6. Sambamba na hilo, takwimu zingine zinazojumuisha kiwango hicho ni kutoka Ulaya Magharibi na Kati (23,400,000 sawa 7.4%), Kusini Mashariki (1,900,000 sawa 2.3%), Ulaya Mashariki (5,500,000 sawa 3.8%), Bara la Amerika (36,700,000 sawa 6.4), Amerika ya Kaskazini (29,400,000 sawa 10.3%), Amerika ya Kusini (7,300,000 sawa 2.6%). Nyingine ni za kutoka Bara la Asia (52,100,000 sawa 2.1%), Australia na New Zealand (3,200,000 sawa 15.3%), Afrika (39,600,000 sawa 8.1%).