Simu kutoka angani
Hivi karibuni abiria wanaweza kuanza kutumia simu zao za mikononi wakiwa katika safari za ndege wanaposafiri katika anga ya nchi za Ulaya.
Wasimamizi kote barani Ulaya wameitisha mashauriano kuhusu uwezekano wa kutumika kwa teknolojia hiyo.
Endapo itaidhinishwa, huduma hiyo itawezesha simu kupigwa tokea angani wakati ndege ikiwa umbali wa mita 3000 juu.
Mashirika ya ndege yatahitaji kuamua endapo yanataka kutumia teknolojia, endapo ruksa itatolewa na idara za usimamizi za nchi husika.
Je mfumo huu unafanyeje kazi?
Kiwango cha ushirikiano kati ya nchi za Ulaya itakuwa na maana kwamba simu za mkononi zinaweza kupigwa wakati ndege zikiruka katika anga za mataifa ambayo bado hayajaidhinisha utekelezaji wa teknolojia hiyo.
Kwa wakati huu matumizi ya simu za mkononi yamepigwa marufuku kwenye ndege kwasababu ya kuwepo kwa ushahidi kwamba zinaweza kuingilia na kuvuruga mawasiliano na mifumo ya kuongozea ndege.
Utafiti uliochatangazwa mwaka 2003 na CAA ulipata matokeo kwamba mawimbi ya simu za mkononi yanavuruga uongozaji wa ndege kwa takriban nyuzi tano.
Hatua tofauti
Msemaji wa taasisi ya usimamizi wa mawasiliano nchini Uingereza ya Ofcom, ameeleza kwamba bado kuna hatua kadhaa kabla ya idhini ya mwisho haijatolewa kuwezesha mpango huo kusambazwa kikamilifu.
Mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa anga ya Uingereza (CAA), na ile ya Ulaya, European Aviation Safety Agency, yanafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba usalama wa ndege na abiria unazingatiwa kabla ya mifumo hiyo kuanza kutumika.
Mawasiliano ya simu za mkononi katika ndege imekuwa kikwazo kwa abiria wengi.
Taasisi ya usimamizi wa ndege imesema kwamba teknolojia hiyo inaweza kuanza kutumika mwaka ujao wa 2008.
Mfumo unaopendekezwa unatumia kituo cha ndani ya ndege ambacho kinarusha mawimbi kwenda simu za mkononi za abiria.
Vituo vya kurushia mawimbi vya simu za mkononi vilivyoko ardhini vitapokea na kusambaza mawasiliano kwa njia ya satellite kuunganisha na vile vya ndani ya ndege.Simu zitatozwa kupitia mitandao ya kawaida ya abiria.
Kwa kuanzia mfumo wa simu utakaotumika ni 2G pekee, japokuwa Ofcom imesema endapo kutakuwa na mafanikio, kutakuwa na uwezekano wa kuzindua kwa mfumo wa kisasa zaidi wa 3G na mingineyo mipya itakayoundwa siku za usoni