Wednesday, November 28, 2007

Dereva amlipua risasi mwenzake wakigombea abiria


Dereva amlipua risasi mwenzake wakigombea abiria
Na Daniel Mjema, Moshi

MFANYABIASHARA wa mabasi yanayofanya safari kati ya Moshi na Kilema, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumpiga risasi, dereva wa basi la Flora Coach kwa madai ya ugomvi wa kugombea abiria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng'hoboko jana aliliambia Mwananchi kuwa, mfanyabiashara huyo ametiwa mbaroni tangu amjeruhi kwa kumpifa risasi mguuni dereva huyo, Rodgers Lyimo, jumamosi iliyopita.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11: 30 jioni katika maeneo ya Kilema Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya basi la mfanyabiashara huyo na lile linaloendeshwa Rodgers aina ya Toyota DCM kufika mwisho wa safari.
" Ni kweli tunaye huyo mfanyabiashara tangu Jumamosi, walizozana na huyo dereva basi
akaamua kuchukua bastola yake na kumpiga risasi ya mguu�tunaendelea kumhoji, " alisema Ng'hoboko.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu kutoka katika Hospitali ya Kilema alikolazwa kwa matibabu, Rodgers alidai kuwa, chanzo cha tukio hilo ni kitendo cha abiria kuteremka kwenye basi la mfanyabiashara huyo na kuingia katika basi analoendesha.
Dereva huyo alidai kuwa, Ijumaa iliyopita majira ya 10:30 jioni, wakiwa katika stendi kuu ya mabasi Moshi, abiria waliingia katika basi lake na kuliacha lile la mfanyabiashara ambalo lilikuwa limepanga foleni mbele yake.
Alisema malalamiko yao, yalifikishwa kwa Meneja wa kituo hicho na kuwasuluhisha kwa
kumuagiza dereva huyo kuwasihi abiria watelemke na kupanda kwenye basi lililokuwa mbele.
" Abiria waliteremka lakini wengi hawakwenda kupanda hilo basi wakasubiri la kwangu
kwa hiyo tukajikuta tumepata abiria mapema na kumpita njiani akiwa bado anatafuta
abiria kitendo ambacho naamini hakikumfurahisha, " alidai.
Dereva huyo, alidai Jumamosi baada ya kumaliza safar,i alimkuta mfanyabiashara huyo katika baa moja iliyopo Kilema na kumsalimia, lakini alikataa kuitikia, akisema alikuwa akimtafuta kwa siku nyingi.
Alidai baadae mfanyabiashara huyo, alimfuata na kumnyang'anya kofia kisha kumpiga
dereva huyo kwa ubao mgongoni na kuanguka na kwamba wakati akiwa katika harakati za kujitetea alimsukuma mfanyabiashara huyo na kuanguka.
"Niliamua kuondoka na kurudi mahali nilipoegesha basi, lakini akanifuata na kuchomoa bastola huku akisema lazima anivunje mguu ili nisimkoroge tena katika kupakia
abiria, "alidai.
Dereva huyo aliongeza kuwa, baada ya kuchomoa bastola, baadhi ya wananchi waliojitokeza kuamua ugomvi lakini walikimbia ndipo mfanyabiashara huyo alimpiga risasi na kutiwa mbaroni baada ya tukio hilo kuripotiwa polisi.

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu