Monday, November 26, 2007

Sakata la upasuaji tata-MOI: Je taratibu hazikufuatwa?



Sakata la upasuaji tata-MOI: Je taratibu hazikufuatwa?
Na Mwasu Sware na Jackson Odoyo.
WASWAHILI husema haraka haraka haina baraka, na mwenda pole hajikwai methali zote zina maana ya kuwa endapo mtu atafanya jambo kwa haraka bila kuzingatia, matokeo yake huwa ni mabaya, na ukifanya jambo kwa uangalifu matokeo yake huwa ni mazuri.
Hivi karibuni kumetokea jambo la kusikitisha ikiwa pia ni la kutatanisha juu ya kuwepo kwa upasuaji tata uliotokea katika Taasisi ya Mifupa (MOI), kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Upasuaji huo ambao uliwahusisha vijana wawili ambao ni Emmanuel Mgaya (19) ambaye alikuwa ana tatizo la kichwa lakini badala yake akafanyiwa upasuaji wa mguu, na yule Emmanuel Didas (20), aliyekuwa na tatizo la mguu alifanyiwa upasuaji wa kichwa.
Kutokana na tukio hilo baadhi ya watu hususan ndugu wa wagonjwa hao wameonekana kusikitishwa, kushangazwa na tukio hilo kiasi kwamba jamii imekuwa na woga dhidi ya huduma ya upasuaji inayotolewa katika Taasisi hiyo.
Akizungumzia tukio hilo lilivyokuwa kwa mtoto wake, mama mzazi wa Emmanuel Mgaya, Mary Mgina anasema, alifika hospitalini hapo akitokea Njombe mkoani Iringa wiki mbili zilizopita kwa lengo la mtoto wake kuja kupatiwa matibabu ya kichwa ambayo yamekuwa yakimsumbua muda mrefu.
�Tumekuja wiki mbili zilizopita tukitokea Njombe katika hospitali ya kibena ambapo tuliandikiwa barua ya kuja huku Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi, mwanangu ameanza kuumwa na kichwa mara baada ya kuanza mtihani wa kidato cha nne akiwa ndani ya chumba cha mitihani shuleni kwake,� anasema mama yake.
Naye mjomba wa Mgaya, Dick Mgina anasema, siku ya kufanyiwa upasuaji mgonjwa wao alichukuliwa kutoka kwenye wodi ya Sewahaji chumba namba 17, na kisha kupelekwa kwenye chumba cha upasuaji, mara baada ya kufanyiwa upasuaji walikuja kukabidhiwa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kichwa lakini hakuwa ndugu yao.
�Tulipokabidhiwa na wauguzi tulimkataa kwa kuwa hakuwa ndugu yetu na hapo ndipo tulipoanza kumtafuta ndugu yetu, katika kumtafuta tulimkuta amefanyiwa upasuaji wa mguu na si kichwa kama ilivyokuwa inatakiwa,�anasema Mgina.
Naye Sisti Marishay ambaye ni kaka wa Emmanuel Didas ambaye amefanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu anasema Didas alifikishwa hospitalini hapo kutokana na kuumia goti baada ya kupata ajali ya pikipiki hivi karibuni na kisha kulazwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI).
Marishay anasema ndugu yake Didas akiwa hospitalini hapo alipigwa picha za x-ray ambazo zilionyesha kuwa hakuwa na matatizo katika mifupa ila alikuwa na uvimbe kwa ndani ndipo madaktari wakashauri afanyiwe upasuaji ili kuondoa uvimbe huo.
Lakini katika hali ya kusikitisha madaktari wakamfanyia upasuaji wa kichwa, wakati hakuwa na tatizo lolote la kichwa, anasema Marishay.
�Naweza kusema kuwa kilichofanyika ni uzembe wa hali ya juu, mdogo wangu alikuwa haumwi kichwa lakini nashangaa amefanyiwa upasuaji wa kichwa na baada ya kutokea tatizo hilo nimezungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Profesa Laurent Museru ambaye alikiri kuwa kuna makosa yametokea hivyo wameamua kukaa na kuunda tume ya kuchunguza uzembe huo, kisha tume hiyo itatoa taarifa baada ya wiki moja,� anasema Marishay.
Wakati huo huo ndugu mwingine Ludani Didas anasema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa mpaka sasa mdogo wake hajitambui, hawezi kuzungumza chochote na yuko ICU, �ni vyema tukasubiri tuone hatima ya Afya yake ndipo nitakapoweza kuzungumzia uzembe huu wa wazi tena wanaofanyiwa wanyonge.�
Baadhi ya wananchi waliozungumzia tukio hilo walisema kwamba tukio hilo linasikitisha na ni vigumu kuelezewa kwa sababu mazingira yaliyo sababisha upasuaji tata huo hayajajulikana japo kuwa inaweza kutafsiriwa kama uzembe wa Wauguzi, Madaktari na idara nzima ya huduma katika taasisi hiyo.
Licha ya jamii kusikitishwa na tukio hilo, wapo pia madaktari bingwa wa upasuaji ambao wameonekana kushangazwa Kutokana na tukio hilo kwa kuwa kabla ya upasuaji wowote kufanyika zipo hatua sita ambazo zinatakiwa kupitiwa na wataalam saba wa afya kabla ya upasuaji.
Madaktari hao wameelezea hatua hizo kuwa ni mgonjwa kupigwa picha ya x-ray kabla ya upasuaji wowote ili kubaini tatizo linalo msumbua baada ya hatua hiyo kuna daktari atakaye husika na upasuaji huo anatakiwa kuisoma x-ray hiyo na kumtambua mgonjwa wake.
Hatua ya pili ni msimamizi wa zamu wodini anatakiwa kuwasiliana kwa karibu na daktari ili kufahamu siku maalum ya kumfanyia mgonjwa huyo upasuaji sanjari na kuwataarifu ndugu wa mgonjwa husika.
Wataalam hao wameongeza kwamba hatua ya tatu ni kumuandaa mgonjwa kwa kumueleza hali halisi ikiwa ni pamoja na kuandaa mahali ambapo anatakiwa kufanyiwa upasuaji huo kama ni kichwani anatakiwa kunyolewa nywele na kufungwa plasta mahali husika.
Hatua ya nne daktari anatakiwa kumuona mgonjwa siku moja ama mbili kabla ya siku ya kufanyiwa upasuaji hatua ya tano ni mgonjwa kutolewa wodini kwenda katika chumba cha upasuaji akiwa na wauguzi wawili na jalada lake kadhalika msimamizi wa zamu wodini na wauguzi hao wawe wamesaini katika faili la mgonjwa.
Wakizungumzia hatua hizo madaktari hao wamesema kwamba hatua ya sita ambayo ni ya msingi zaidi ni wakati wauguzi wa wodini wanapokabidhiwa mgonjwa, kabla ya kumpokea wanapaswa kumkagua kwanza kama ameambatana na vibali vyake vyote na kumtambua kwa kumuita majina yake mawili kama ni mgonjwa anayeweza kuzungumza.
Wamefafanua kwamba kama hawezi kuzungumza wanapaswa kuwauliza ndugu wa mgonjwa kwa sababu wanapaswa kuwepo kwani ni makosa kumuondoa mgonjwa wodini na kumpeleka katika chumba cha upasuaji bila ndugu zake kufahamu wala kuwapo.
Baada ya hatua hiyo wauguzi hao wanapaswa kusaini kabla ya kumuingiza mgonjwa katika chumba hicho hata hivyo wamesema kwamba mgonjwa akisha ingizwa katika chumba cha upasuaji daktari wa usingizi anapaswa kumkagua mgonjwa na kuzungumza naye ama kuzungumza na ndugu zake ili ahakikishe kwamba huyo ndiye.
Ndipo daktari wa upasuaji anamkagua na kuzungumza naye kwa mara nyingine huku akimuondolewa wasiwasi ili mgonjwa aweze kumzoea na hata atakapo zinduka baada ya upasuaji awe anauwezo wa kukumbuka mambo aliyozungumza mara ya mwisho kabla ya kuchomwa sindano ya usingizi sanjari na kumkumbuka daktari wake.
Wameeleza kwamba baada ya hapo ndipo mgonjwa huyo anapaswa kuchomwa sindano ya usingizi (nusu kaputi) kisha ndipo daktari aanze kazi ya kumpasua mgonjwa huyo. Wanasema kuwa kwa kupitia hatua zote hizo si rahisi makosa kama hayo kutokea japokuwa ni makosa ya kibinadamu lakini pia wanapaswa kuzingatia kanuni zote hizo ili kuepukana na makosa kama hayo.
Madaktari hao wameeleza kwamba hilo si tukio la kwanza kutokea katika taaluma yao, ila huenda likawa ni la kwanza masikioni mwa Watanzania hivyo limeweza kusababisha mfadhaiko hususan kwa wale waliopatwa na tukio hilo.
Wamesema kwamba kila daktari anapenda mgonjwa wake apone na inapotokea vinginevyo huwa wanakosa raha, wakati mwingine wanarudi nyumbani wakisikitika huku wakipekua upya kurasa za vitabu ili wafahamu sababu zaidi inayomfanya mgonjwa asipone.
�Sasa kutokana na kanuni na baadhi ya taratibu hizo, daktari hawezi kufanya kosa kubwa kama hilo, sisi tuna wasiwasi kwa nini tukio kubwa kama hilo limetokea kama kweli wataalamu wote walifuata kanuni hizo, wanasema madaktari hao bingwa�.
Pia kuna kanuni zilizowekwa kitaalamu kabla ya kumfanyia upasuaji mgonjwa, lakini siku hizi watu wamezoa kufuata njia za mkato badala ya kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa kitaalamu kwa ajili ya upasuaji.
Na kuwa linapotokea tatizo kwa upande wa afya kuna njia tatu ambazo wasimamizi wa vitendo wametakiwa kuzifuata kabla ya kuchukua hatua yoyote.
�Linapotokea tatizo la afya kuna njia tatu ambazo wasimamizi wa vitengo wanatakiwa kuzifuata kabla ya kuchukua hatua yoyote ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa Wizarani, kuwasilisha taarifa baada ya kufanya uchunguzi wa tatizo hilo na kisha Baraza la Madaktari linapaswa kuketi kwa ajili ya kujadili na kutoa taarifa yake,� wanasema madaktari hao.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, Novemba 8 ilibainika kuwa, Daktari aliyepangwa kupasua hakutokea, alikuwa na udhuru. Pia mgonjwa aliyetakiwa kufanyiwa upasuaji wa kichwa hakuwa amenyolewa nywele na badala yake, wauguzi walifanya kazi hiyo baada ya kuulizwa.
Vilevile ilibainika kuwa, Daktari aliyesimamishwa kazi baada ya kufanya upasuaji tata huo siku ya tukio hakuwa zamu ila alifika hospitalini hapo kwa lengo la kumzibia pengo daktari aliyetakiwa kufanya upasuaji.
Uchunguzi huo pia ulibaini kuwa, Daktari huyo hakuwahi kumuona mgonjwa kabla ya kumfanyia upasuaji na kwamba alipoingia kwenye chumba cha upasuaji, alikuta mgonjwa ameshapigwa sindano ya nusu kaputi.
Mara baada ya Daktari huyo kukamilisha upasuaji huo alimkabidhi mgonjwa kwa wauguzi ili wamrudishe wodini.
Sasa kutokana na kusimamishwa kwa daktari huyo ambaye ndiye bingwa wa upasuaji wa kichwa kumekuwapo na msongamano mkubwa wa wagonjwa kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa msimamizi wa madaktari wengine wakati wa upasuaji.
Kutokana na tukio hilo, mnamo Novemba 6, Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Profesa Laurent Museru aliagiza kuundwa kwa tume ili kuchunguza kwa undani tukio la wagonjwa hao.
Tume hiyo ambayo ina wajumbe sita, inaongozwa na Profesa Victor Mwafongo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kuwapo kwa tume hiyo itasaidia Serikali kuchukua hatua zinazotakiwa endapo watu watabainika kutenda kosa ama kufanya uzembe uliosababisha kosa kutendeka.
Akizungumza ofisini kwake Mganga Mkuu wa Serikali, Deo Mtasiwa alisema, Serikali haiwezi kupuuza tukio hilo, lakini inahitaji kupata taarifa za kweli.
�Tunaitaka tume ifanye kazi hiyo haraka, kisha kuleta majibu ili tuweze kutoa tamko mara moja,� alisema Dk. Mtasiwa.
Naye, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa amesema amewataka wananchi wasubiri taarifa kamili itakayotolewa na tume na kisha kutoa rai kwa vyombo vya habari huku akisisitiza kuwa jambo hili ni zito hivyo ni vyema lizungumzwe kwa undani.
Mwakyusa anasema upotoshaji unaweza kuleta hofu isiyo ya kawaida kwa wananchi.

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu