Tuesday, December 11, 2007

ATC aibu!





ATC aibu!

2007-12-10 17:16:36
Na Mwandishi wa Alasiri Jijini

Shirika la Ndege nchini, ATC limelaumiwa kwa kufanya kitendo cha aibu ya mwaka kwa kuwasotesha kwa wiki nzima mahujaji zaidi ya 300 ambao wameshakamilisha taratibu zote za safari.

Aidha, Shirika hilo limetakiwa kuwalipa fidia mahujaji hao kutokana na gharama walizoingia mara kadhaa wakati wakifika uwanjani hapo ili wasafiri, na kisha kuishiwa kupewa kauli za ‘njooni kesho, rudini kesho kutwa.

Aliyetoa kauli hiyo ya kulaani kitendo cha ATC na kukiita kuwa ni cha aibu ni Kiongozi wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda.

Ni aibu na fedheha... Serikali inapaswa kuwajibika kwa sababu, kama ndege iliyotegemewa imeharibika, ni yenyewe ndiyo inayopaswa kuingilia kati na kuokoa adha wanayoipata waisilam hawa ambao wameshalipia kila kitu, akasema Sheikh Ponda.

Kama si Serikali kuingilia, nani sasa atakayewezesha mahujaji hawa kulipia gharama kubwa walizoingia kwa kukaa jijini zaidi ya wiki sasa, wakiishia kila siku kusoteshwa Airport kwa kuahidiwa safari?

Ni vyema gharama hizi zikafidiwa na wahusika wanaotoa taarifa zisizokuwa na ukweli, tena zaidi ya mara moja, wawajibishwe, akaongeza Sheikh Ponda.

Aidha, katika orodha ya mahujaji waliosoteshwa zaidi ya wiki moja sasa pale katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, inaelezwa yumo baba mkwe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Jakaya Kikwete na mashemeji zake kadhaa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ni kwamba, kama walivyo mahujaji wengine, ba`mkwe huyo mzaa chema wa Rais Kikwete aitwaye Mzee Rashid Yusuph Mkwachu, ametaabika mno na njoo kesho ya ATC.

Pia waliokumbwa na adha hiyo inayodaiwa kusababishwa na ubovu wa ndege iliyotegemewa kusafirisha mahujaji hao huku zikitolewa ahadi hewa za kila mara ni shemejie Rais Kikwete aitwaye Mwanakombo Bakari na ndugu wengine ambao ni Hassan Mohamed na Jamillah Omar.

Imedaiwa kuwa mahujaji hao walikuwa wasafirishwe wiki iliyopita na ATC, lakini wakaishia kurudishwa na kuahidiwa kila mara kuwa watasafirishwa, lakini bila ya mafanikio.

Jana usiku, imeelezwa na Sheikh Ponda kuwa taarifa walizopelekewa na Mwenyekiti wa Bodi ya ATC ni kwamba sasa, safari hiyo iliyoahirishwa tena jana, itakuwa leo jioni.

  • SOURCE: Alasiri
Tuma Maoni Yako
Posted by Picasa

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu