|
---|
Habari za Kitaifa | | Serikali yaokoa mahujaji | Waandishi Wetu HabariLeo; Wednesday,December 12, 2007
| SERIKALI jana iliwaokoa mahujaji zaidi ya 1,150 waliokuwa wamekwama Dar es Salaam kwenda Makka na Madina, Saudi Arabia, baada ya kuwakodia ndege kwa ajili ya kwenda huko kuhudhuria ibada hiyo muhimu katika dini ya Kiislamu.
Hatua hiyo ilikuja baada ya mahujaji hao, wengi wao wakiwa ni Watanzania na wengine kutoka Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), kukwama Dar es Salaam kwa zaidi ya siku 10, baada ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), kushindwa kupata ndege ya kuwasafirisha kama ambavyo walikubaliana baada ya kulipa dola za Marekani 2,400 (takriban Sh milioni tatu).
Awali ndege ya kwanza ya kukodi ya ATC ilitarajiwa kuondoka Dar es Salaam Desemba 3, mwaka huu, lakini ndege hiyo aina ya Boeing 747-200 kutoka Uarabuni, haikuweza kuruka kutokana na hitilafu, na kuanzia siku hiyo zimekuwapo taarifa za kuchanganya kuhusu safari hiyo.
Kufikia saa 12:15 jioni, kundi la kwanza la mahujaji 379, lilitakiwa kuingia ndani ya sehemu ya kukaguliwa tayari kwa safari ya Makka ambayo leo usiku ndiyo siku ya mwisho ya kuingia katika miji hiyo mitakatifu kwa ajili ya ibada hiyo ambayo ni nguzo ya tano katika dini ya Kiislamu. Ndege aina ya DC 10, ilikuwa imetua uwanjani hapo tayari kuwachukua mahujaji hao.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, ndiye aliyewatangazia mahujaji hao kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kuwa safari hiyo ipo, baada ya awali asubuhi kuwaeleza kuwa serikali ipo pamoja nao, na aliwahakikishia itafanya kila linalowezekana kuhakikisha haiwaangushi.
Akifuatana na Mwenyekiti wa Bodi ya ATC, Balozi Mustafa Nyang’anyi, Mkurugenzi Mkuu wa ATC, David Mattaka na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Lindi na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania, Sheikh Suleiman Gorogosi, Kandoro alisema mahujaji hao wote wataondoka, hata kama siyo wote kwa jana usiku.
“Kundi la kwanza litaondoka sasa (saa 12 jioni) na jingine litaondoka kwa ndege itakayokuja baadaye. Hata kama ndege nyingine haitakuja, ndege hii inayoondoka sasa itakwenda na kurudi kwa sababu marubani tumewapanga kwa makundi. Kwa hiyo hakuna atakayebaki hapa,” alisema Kandoro.
Alisema serikali haikuingia awali katika mgogoro huo wa ATC na mawakala wa mahujaji hao, kwa sababu walifahamu suala hilo lingemalizwa kati yao, na ndiyo maana iliamua kuingilia kati baada ya kuona tatizo hilo linashindwa kupata ufumbuzi.
Kandoro alitangaza utaratibu huo muda mchache kabla ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kufika uwanjani hapo kuagana na mahujaji hao na kuwatakia safari njema.
Awali, juzi kulikuwapo na kikao kirefu kati ya viongozi wa ATC na wawakilishi wa mahujaji, na baada ya kikao hicho, mahujaji waliarifiwa kuwa kundi la kwanza la mahujaji hao lingeondoka jana na ndege aina ya TC- 8000 ambayo ilitarajiwa kufika majira ya saa 3:30 asubuhi na kuondoka jana majira ya saa 5:00 asubuhi. Lakini mpaka kufikia saa 9:00 alasiri, hakuna ndege yoyote iliwasili.
Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ambaye ATC iko chini ya Wizara yake, alifika uwanja wa ndege jana asubuhi, lakini hakuzungumza lolote kuhusiana na suala hilo, ingawa taarifa zilieleza kwamba ndiye aliyekuwa akihangaika kuhakikisha mahujaji hao wanaondoka jana usiku.
Hata hivyo, jana saa nne asubuhi, mahujaji walifanya mkutano na kuamua kwamba endapo hawatasafiri kwa jana hiyo wangefanya maandamano makubwa ya kupinga na kulaani kitendo hicho.
“Tutaandamana ili kukomesha taratibu zote za uongo na tunataka iwe funzo, wajue kuwa tumeumia na tunapinga kitendo hicho”, alisema Seif Llah, mmoja kati ya viongozi watatu wanaowakilisha makundi yote ya mahujaji, walioteuliwa juzi usiku baada ya mahujaji kukosa imani na viongozi wao waliokuwamo kwenye mkutano na viongozi wa ATC pamoja na serikali.
Katika hatua nyingine, mahujaji hao waliochelewa kwenda Makka na Madina, wana haki ya kuidai ATC fidia isiyozidi dola 5,000 za Marekani kila mmoja kwa kucheleweshewa safari yao.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga, Mustapha Akonay, alilieleza gazeti hili Dar es Salaam jana kuwa hata kama wamesafiri, walicheleweshwa, hivyo wana haki ya kudai fidia hiyo. Akonay alisema kwa kuwa mahujaji walikuwa wanakwenda nje ya nchi, Mkataba wa Montreal wa mwaka 1999 ulioridhiwa na Serikali ya Tanzania, Februari 2003 unawatambua kuwa ni abiria wa kimataifa, hivyo wana haki kisheria kudai fidia hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha mkataba huo.
Katibu wa baraza hilo, Hamza Johari, alisema jana kuwa, hakuna muda maalumu kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga kudai fidia hivyo wanaweza kudai fidia wakirudi. Alisema mahujaji wakihitaji kulipwa fidia watapaswa kuidai ATC moja kwa moja na wawasilishe nakala za madai yao katika baraza ili liwe na taarifa za kuwapo kwa madai hayo.
Kwa mujibu wa taratibu, anayedai fidia anapaswa kuwasilisha madai kwa maandishi, waeleze kilichotokea, waeleze mdaiwa afanye nini sambamba na kutaja kiasi cha fidia anachotarajia kulipwa.
Akonay alisema baraza limewasiliana na uongozi wa juu wa ATC hivyo wanasubiri maelezo ya shirika hilo kuhusu namna walivyoshughulikia tatizo hilo.
Kwa mujibu wa Akonay, Jumatatu mchana alimpigia simu Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATC, David Mattaka, kumuuliza kuwa shirika linafanya nini kutatua tatizo hilo. “Yeye alisema tunashughulikia, tutawajulisha matokeo,” alisema Akonay. | | | | |
|
---|
|
---|
| Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved |
|
---|
|
|