Monday, November 19, 2007

Kikwete amkaanga Zitto









na Charles Mullinda
SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuwa mjumbe katika Kamati ya Kupitia Mikataba ya Madini, dalili za awali zimeonyesha kuwa, uteuzi huo utamgharimu kisiasa mwanasiasa huyo kijana.
Habari za uhakika zilizolifikia Tanzania Daima Jumapili, zinaeleza kuwa uteuzi wa Zitto katika kamati hiyo umewashitua baadhi ya viongozi wakuu serikalini na tayari wamekwishawaagiza wapambe wao kumshughulikia mbunge huyo.
Imeelezwa kuwa, wasiwasi huo wa wakubwa serikalini, unatokana na shaka kwamba, Zitto anaweza kuwa mwiba kwa udhaifu utakaobainika katika mikataba hiyo, kwa kuanika hadharani kila kitakachogunduliwa na kamati, hata kama atatakiwa kutofanya hivyo.
Hata hivyo, wadadisi wa mambo wanaeleza kuwa, hatua ya Rais Kikwete kumteua Zitto kwenye kamati hiyo, inalenga kuwapa mwanya wanamtandao kumshughulikia mbunge huyo anayeonekana kuitikisa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Habari zaidi zinaeleza kuwa, Rais Kikwete ameshitushwa na mwenendo wa mambo ndani ya serikali na katika CCM, na kwamba kwa kiasi kikubwa umaarufu wa serikali yake umekuwa ukipungua, huku ule kambi ya upinzani ukizidi kuongezeka.
Kwamba Rais Kikwete kwa siku kadhaa amekuwa katika hali ya woga, hasa baada ya matukio ya kuzomewa kwa mawaziri wake, huku viongozi wengine wa serikali wakipigwa mawe na kuzodolewa na wananchi wanaoonekana kukata tamaa na uongozi wa serikali yake.
Taarifa nyingine zilizopatikana kutoka ndani ya kundi la wanamtandao zinaeleza kuwa, woga alionao Rais Kikwete dhidi ya kupanda kwa umaarufu wa kambi ya upinzani katika siku za hivi karibuni, ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na Zitto, umemfanya abuni mbinu mpya za kukabiliana na hali hiyo.
Mbinu ya hivi karibuni inayoelezwa kuwa imebuniwa na Rais Kikwete kuanza kumshughulikia Zitto, ni kumshirikisha katika tume hiyo ili akose sauti kubwa ya kukosoa udhaifu uliomo ndani ya mikataba ya madini.
Wachambuzi wa duru za kisiasa wanadai kwamba, serikali baada ya kushindwa kumbana Zitto kupitia Bunge, ambako Waziri Mkuu, Edward Lowassa aliongoza mikakati hiyo kwa kuwaita wabunge wa CCM na kuwataka waweke msimamo wa pamoja wa kumshughulikia mwanasiasa huyo, na kwa kauli moja waliafikiana kumsimamisha kufanya shughuli za Bunge, Rais Kikwete alianza kupata hofu dhidi ya mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, hasa baada ya umaarufu wa kambi ya upinzani kuanza kupanda.
Wanaeleza zaidi kwamba, baada ya vuguvugu la wananchi kuwa kubwa kufuatia kusimamishwa kwa Zitto, serikali ilibuni mbinu kadhaa za kulinyamazisha, zikiwemo ziara za mawaziri mikoani kupambana na hoja za kambi ya upinzani.
Hata hatua ya Rais Kikwete kumtetea Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ambaye aliliambia Bunge kuwa mikataba yote ya madini imeshapitiwa, nayo inadaiwa kuwa moja ya mbinu za kupambana na hoja ya Zitto aliyoiibua bungeni.
Kushindwa kufanikiwa kwa mbinu hizi, ndiko kulikomfanya Rais Kikwete kubuni mbinu ya kuunda Kamati ya Kuchunguza Mikataba ya Madini, mbinu ambayo imeanza kuonyesha mafanikio.
Kwa kutumia mbinu hii, vijana wa kundi la ‘wanamtandao maslahi’ walio katika fani ya uandishi wa habari, walimhoji Zitto baada ya kutangazwa kuwa ni mmoja kati ya wajumbe wa kamati hiyo na kumnukuu akieleza kuwa Rais Kikwete ni rais makini anayepaswa kuliongoza taifa hili kwa sasa.
Kauli hii ya Zitto, inamuonyesha kuwa kiongozi kigeugeu ambaye hivi karibuni alikuwa mstari wa mbele, pamoja na viongozi wengine wa kambi ya upinzani kumlaumu Rais Kikwete kwa kushindwa kutekeleza baadhi ya ahadi zake kwa Watanzania, pamoja na kumtaja katika orodha ya watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Hata hivyo, baadhi ya watu walio karibu na mwanasiasa huyo, walilieleza gazeti hili kuwa, ingawa kweli Zitto alihojiwa na waandishi na habari, baadhi ya maneno yaliyoandikwa hakuyatamka, bali yameandikwa kwa lengo la kumshushia heshima yake kwa jamii.
Hatua nyingine inayodhihirisha kufanikiwa kwa mbinu hiyo, ni mgongano wa kauli za viongozi wa CHADEMA. Wakati Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe akipinga waziwazi kuteuliwa kwa Zitto katika kamati hiyo na akimtaka kujitoa mara moja, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbroad Slaa, yeye ameeleza kuwa chama kinaunga mkono kuteuliwa kwa Zitto.
Habari za hivi karibuni zilizolifikia Tanzania Daima Jumapili zinaeleza kuwa, baadhi ya viongozi wa chama hicho usiku wa kuamkia jana walifanya kikao kizito cha dharura cha kujadili uteuzi huo wa Zitto.
Wakati hali ya mambo ikiwa hivyo ndani ya CHADEMA, wananchi mbalimbali waliotoa maoni yao kuhusu uteuzi huo, wameonyesha shaka ya wazi kuwa huo ni mwanzo wa kumshughulikia Zitto na kauli yake kukubali uteuzi huo na kummwagia sifa Rais Kikwete ikichukuliwa kama shukrani kwa rais kumkumbuka kuwemo katika kamati hiyo.
Rais Kikwete alitangaza kamati hiyo hivi karibuni na itaongozwa na Mwanasheria Mkuu mstaafu, Jaji Mark Bomani.
Wengine kwenye kamati hiyo itakayofanya kazi kwa miezi mitatu, ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM) ambaye ni Mbunge wa Kyela na Ezekiel Maige kutoka Jimbo la Msalala (CCM).
Wajumbe wengine ni Peter Machunde wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, David Tarimo wa PriceWater Coopers, Maria Kejo wa Wizara ya Sheria na Katiba, Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Salome Makange, Mugisha Kamugisha kutoka Wizara ya Fedha na Edward Kihundwa, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Makazi, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu