Friday, November 23, 2007

Tiba MOI:Aliyepasuliwa mguu badala ya kichwa, afariki










Tiba MOI:Aliyepasuliwa mguu badala ya kichwa, afariki

Jackson Odoyo na Andrew Msechu


EMMANUEL Mgaya (19), aliyefanyiwa upasuaji wa kichwa Jumatatu wiki hii baada awali kufanyiwa wa mguu kimakosa, katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), amefariki dunia jana asubuhi.
Mara baada ya Mgaya kufanyiwa upasuaji wa kichwa, hali yake ilibadilika na kuwa mbaya kisha kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), hadi mauti yalipomfika jana saa 2:30 asubuhi.
Awali Mgaya alifanyiwa upasuaji wa mguu badala ya kichwa na Emmanuel Didas ya kichwa badala ya mguu, Novemba mosi mwaka huu katika taasisi hiyo.
Akizunguza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu muda mfupi baada ya Mgaya kufariki dunia, mmoja wa wauguzi wa MOI, alisema hali ya mgonjwa huyo, ilianza kuwa mbaya juzi mchana.
Alisema jana asubuhi mapema alipofika kazini, alimkuta akipumua kwa shida, hali iliyoonyesha alikuwa amezidiwa.
Aliongeza kuwa, baadaye madaktari wanaomuhudumia waliwasili katika chumba hicho na kugungua hali yake ilikuwa ni mbaya zaidi.
Hali ya mgonjwa huyo ilianza kuwa mbaya tangu jana (Juzi)mchana na niliporudi kazini leo (jana)alfajiri nilikuta hali yake imebadilika kiasi cha kunipa wasiwasi, lakini madaktari walifika muda mfupi badaye na kumpa huduma za haraka japo hazikuweza kumsaidia, � alisema muuguzi huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini kwa kuwa si msemaji.
Kwa mujibu wa chanzo, jitihada za kuokoa maisha ya Mgaya zilishindika majira ya saa 2:30 mgonjwa huyo alifariki dunia.
Hata baadhi ya madaktari waliozungumza na Mwananchi walithibitisha kwamba Mgaya amefariki dunia.
�Kifo cha Mgaya kimetushutua sana kwa sababu tangu alipofanyiwa upasuaji wa mara ya kwanza kila daktari wa taasisi hii alijaaribu kumsaidia kwa karibu, � alisema daktari huyo.
Waliongeza kwamba hata Mkurugenzi Mkuu wa MOI, Profesa Laurent Museru, amesikitishwa sana na kifo hicho na kulazimika kuitisha kikao cha dharura kujadili namna ya kufikisha taarifa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kwa ndugu wa marehemu huyo.
Akizungumza na Mwananchi, Profesa Museru amethibitisha kutokea kwa kifo cha Mgaya.
�Ni kweli Mgaya alifariki dunia leo (jana) asubuhi na tumeshawajulisha ndugu zake pamoja kutoa taarifa wizarani, pia mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti,alisema Profesa Museru.
Alisema kwamba utaratibu wa maziko yake, utafahamika baada ya kuwasiliana na ndugu zake. Mgaya ni mwenyeji wa Mkoa wa Iringa.
Habari za kifo cha Mgaya, si tu zimewashtusha wafanyakazi wa MOI, pia Waziri wa Afya, kimesema chanzo chetu cha habari.
Mgaya alifikishwa katika taasisi hiyo, Oktoba 28, mwaka huu akitokea mkoani Iringa na kufanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu matatizo yake na madaktari kushauri afanyiwe upasuaji wa kichwa.
Mwanzoni mwa mwezi huu, badala ya kufanyiwa upasuaji wa kichwa, alifanyiwa upasuaji wa mguu, huku Didas akifanyiwa wa kichwa badala ya mguu.
Kwa sasa Didas amelazwa ICU katika taasisi hiyo huku kukiwa na habari kwamba amepoza upande wa kulia wa mwili.
Tokea Didas amefanyiwa upasuaji huo tata, hajaamka, wala hajaongea na kadri siku zinavyokwenda hali yake, inazidi kuwa mbaya.
Baada ya tukio hilo, Prof Museru aliamriwa na Bodi ya MOI, kuunda tume ya kuchunguza upasuaji huo na kutekeleza hilo, Novemba 2 mwaka huu.
Tume ilikamilisha kazi yake Novemba 13, na kuikabidhi Bod Novemba 15, na Bodi kuipeleka kwa Waziri Novemba 16.
Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyusa ameahidi kutoa taarifa ya Tume hiyo iliyoundwa kuchunguza sakata la upasuaji huo.
Taarifa iliyopatikana jana kutoka katika wizara yake, ilifahamisha kuwa, Profesa Mwakyusa anatarajiwa kutoa taarifa hiyo leo saa 4.00 wizarani hapo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa vya upimaji kwa ajili ya wagonjwa wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) jijini Dar es Salaam jana, Mwakyusa aliahidi kutoa taarifa hiyo leo, baada ya kumalizia maandalizi ya mwisho.
Naombeni munivumilie kwa leo, ninamalizia utaratibu wa kuitoa, ila nitaitoa kesho , siewezi kuzungumza lolote leo kwa kuwa ninaweza kuzungumza nusu nusu, nivumilieni kama mlivyonivumilia tangu nilipowaomba kufanya hivyo nilivyokuwa Bungeni Dodoma, � Waziri huyo aliwaambia wanahabari waliotaka kujua hatma ya taarifa hiyo.
Alisisitiza kuwa, subira ni suala la msingi, hivyo wanachi hawana budi kusubiri kwa muda ili waweze kupata taarifa iliyokamilika.
Awali Prof Mwakyusa, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari, akisema taarifa hiyo angeitoa juzi, lakini kwa sababu zisizojulikana, alishindwa kufanya hivyo.

Dk. Rashid aombwa arejee Tanesco



Waandishi WetuHabariLeo; Friday,November 23, 2007 @00:04
BODI ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania inambembeleza aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dk. Idris Rashid aliyejiuzulu juzi, atengue uamuzi wake, imefahamika. Ingawa mamlaka zinazohusika hazikutaka kusema lolote kuhusiana na suala hilo lakini chanzo chetu cha habari kimethibitisha kuwa bado inamsihi Dk. Rashid abadili uamuzi wake. "Ni kweli tuko katika jitihada hizo za kuzungumza naye kuona kama atabadilisha uamuzi wake," alisema mjumbe mmoja wa bodi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini. Dk. Rashid mwenyewe alipoulizwa kama amepokea maombi ya bodi ya kumtaka abadilishe uamuzi wake aligoma kuzungumzia kujiuzulu kwake na kusema atatoa tamko muda mwafaka ukifika. “Nimepokea simu nyingi kutoka kwa waandishi wa habari tangu asubuhi na jibu langu ni lilelile … sina cha kusema, tafadhali naomba respect (heshima)!” alisema Dk. Rashid ambaye alijiuzulu juzi jioni. Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Balozi Fulgence Kazaura alipoulizwa kama bodi hiyo ina mpango wa kumshawishi Dk. Rashid atengue uamuzi wake alisema: “Sina taarifa hiyo,” alisema. Kazaura alisema kuwa Dk. Rashid aliomba mwenyewe kujiuzulu juzi wakati wa Kikao cha Bodi bila kutoa sababu za hatua hiyo. “Hakusema kwa nini anajiuzulu lakini aliishukuru bodi kwa msaada iliyompa tangu aje kusaidia kuliboresha Shirika,” alisema Kazaura kwa sauti ya jazba na kumkatia simu mwandishi baada ya kumtaka aeleze sababu za mkurugenzi huyo kujiuzulu. Akizungumza na gazeti hili Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, alisema uamuzi wa mkurugenzi huyo hauwezi kuingiliwa na serikali kwa sababu yupo chini ya bodi lakini alikiri kupokea barua ya kujiuzulu kwa saa 24 kutoka kwa mkurugenzi huyo jana. “Ingekuwa amefukuzwa tungekuwa na maelezo ya kutoa lakini kwa sababu amejiuzulu mwenyewe maelezo yote yanapatikana kwa bodi lakini mimi nimepokea barua yake inayoeleza amejiuzulu,” alisema Waziri Karamagi ambaye hakuwa tayari kueleza zaidi. Naye Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema serikali kwa sasa haiwezi kuzungumza lolote hasa kutokana na nafasi ya Rais kuwa mteuzi tu na kwamba kwa suala la kujiuzulu linaigusa moja kwa moja Bodi ya Tanesco ambayo ndiyo inayoripoti kazi kwake. “Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco anaripoti kazi kwa bodi hivyo Rais yeye ni mteuzi tu wa anayeshika nafasi hiyo, hawezi kuingilia chochote. Nadhani bodi inahusika moja kwa moja na suala hili,” alisema Rweyemamu. Meneja Uhusiano wa Shirika hilo, Daniel Mshana alisema jana kuwa ni mapema kuzungumzia suala hilo na kuongeza kuwa kama kutakuwa na taarifa zozote kwa umma zitatolewa kwa wakati mwafaka. Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Tanesco, Stephen Mabada ambaye amekuwa anafanya kazi kwa karibu na Dk. Rashid alipoulizwa hali ikoje kwa wafanyakazi alisema ni ya kawaida na walikuwa wanaendelea kuchapa kazi kama kawaida. Licha ya mamlaka husika kutotaka kueleza sababu ya mkurugenzi huyo kujizulu, lakini baadhi ya vyanzo vya habari vimekuwa vinaeleza kuwa yeye ndiye aliyeshinikiza umeme kukatwa katika Kiwanda cha Saruji cha Tanga kutokana na kudaiwa Sh milion 49. Lakini bodi ilipingana na uamuzi wake ikieleza kuwa kiwanda hicho ni miongoni mwa wateja wakubwa lakini pia kinalipa kodi kubwa kwa serikali. Katika hali hiyo Dk. Idris akaona hawezi kufanya kazi katika mazingira ya ushauri wake kupingwa. Sababu nyingine inayotajwa kujiuzulu kwa mkurugenzi ni mpango wa shirika hilo kutaka kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 40 na gharama za ufungaji kwa wateja wapya zaidi ya asilimia 150. Kuna madai kuwa bodi haikukubaliana na mpango huo kwa madai kuwa utawaumiza wananchi. Dk. Rashid aliteuliwa kushika wadhifa huo Novemba mwaka jana baada ya menejimenti ya Netgroup ya Afrika Kusini kumaliza muda wake Desemba 31 mwaka jana baada ya kuiongoza TANESCO kwa takriban miaka minne mfululizo kuanzia Mei, mwaka 2002. Wakati anatangaza uteuzi wake Balozi Kazaura alimwelezea Dk. Rashid, ambaye aliwahi kuwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT) kati ya mwaka 1993 na 1998, kuwa mchumi kutokana na kuwa na Shahada ya Udaktari katika masuala ya Uchumi (PhD-Economics) aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Boston, Massachusetts, nchini Marekani, Juni, 1984. ’’Uteuzi wa Dk. Rashid, umezingatia umuhimu wa kuwa na mtu mwenye uwezo mkubwa wa kusimamia masuala ya kifedha na pia ambaye ana uzoefu wa muda mrefu katika shughuli za menejimenti,’’ ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Dk. Rashid pia aliwahi kuwa bosi NBC, Gavana wa BoT baada ya mkataba wake kumalizika hakutaka kuendelea badala yake akaenda kuongoza benki binafsi ya Akiba. Pia amewahi kuwa bosi wa Kampuni ya Simu ya Vodacom katika benki ya makabwela ya NMB na baadaye akateuliwa kuiongoza Tanesco wakati huo ikiwa taabani kifedha. Wachambuzi wa mambo waliotoa maoni yao kwa gazeti hili baadhi yao wamemsifu Dk. Rashid kwa kujiuzulu kwake kwani ameonyesha uadilifu wake kwa kuamua kuachia ngazi baada ya kuona mambo hayaendi ndani ya shirika hilo. Wengi wao wamekuwa wanaeleza kuwa huenda mtaalamu huyo wa mambo ya uchumi kaachia ngazi baada ya kuona kuna siasa katika uendeshaji wa shirika hilo. Wadau wengine wanafurahia kujiuzulu kwake kwa madai kuwa kama kweli ndiye aliyekuwa anang'ang'ania shirika hilo lipandishe gharama hizo hakuwa anajali wananchi walio wengi. "Huwezi kupandisha gharama ya umeme kwa asilimia 40 na huduma nyingine zaidi ya asilimia 100 bila kuwaonyesha watu kwanini unafanya hivyo." Dk. Rashid amejiuzulu wakati shirika hilo likiwa katika harakati za kupandisha gharama zake jambo ambalo linalalamikiwa na wananchi walio wengi. Leo wananchi wa Dar es Salaam watatoa maoni yao kuhusiana na mpango huo wa Tanesco. Wengine wanaeleza kuwa Tanesco inasema iko katika hali mbaya kwa sababu haikuwa ikikusanya madeni yake serikalini na katika mashirika ya umma na kwa kampuni binafsi, watumishi walikuwa wakiachia umeme huku wao wakikusanya fedha.

Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu