Wednesday, November 21, 2007

Vyama vya upinzani CUF, TLP vyajadili kuhusu Zitto





















Vyama vya upinzani CUF, TLP vyajadili kuhusu Zitto

*Wawaasa Chadema wazungumzie hoja ya msingi

* Wasema mjadala ulenge katika rasilimali za nchi

*Makani ataka Zitto aingie jikoni kupakua ukweli

Na Waandishi Wetu


VYAMA vya CUF na TLP, vimewataka viongozi wa Chadema kuacha kujadili uteuzi wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe katika kamati ya kuangalia upya mikataba ya uchimbaji madini nchini na badala yake kisisitize mjadala katika hoja ya msingi.
CUF na TLP, vimesema wanachopaswa Chadema na jamii kwa jumla hivi sasa ni kukijadili kuhusiana na suala zima la ufisadi katika rasilimali za nchi, badala ya kumjadili Zitto.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TLP Taifa Augustine Mrema, alisema kuwa Chadema na jamii hawapaswi kumzungumzia Zitto, badala yake wanachotakiwa kukifanya ni kuzungumzia hoja ya msingi na kutokubali kutolewa nje ya hoja hiyo.
�Ikiwa jamii na viongozi wa Chadema watakubali kutolewa nje ya hoja ya msingi ya ufisadi na kuingizwa katika kumjadili Zitto watakuwa wamekosea,� alisema Mrema.
Alisema uteuzi wa Zitto katika kamati hiyo sio suala la kujadili kwani angeweza kuchaguliwa yeyote, bali linalopaswa kujadiliwa ni dhamira ya Rais Jakaya Kikwete ya kuunda kamati hiyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Bindamu na Mahusiano na Umma wa CUF, Mbaralah Maharagande, alisema maoni tofauti yanayotolewa na viongozi wa Chadema kuhusiana na uteuzi wa Zitto kwenye kamati hiyo, ni ya mtu mmoja mmoja na sio kauli ya pamoja.
Alisema kinachopaswa kujadiliwa hivi sasa, ni kuhusu ufisadi katika matumizi ya rasilimali za nchi, mikataba yenye utata ya uchimbaji wa madini, ikiwa ni sehemu moja tu ya ufisadi huo hapa nchini.
�Suala sio kujadili uteuzi wa Zitto katika kamati ya madini, tusikubali kuchezewa hisia zetu kwa kutolewa nje ya hoja kuu, suala ni kwamba kamati haiwezi kutoa matunda yaliyokusudiwa�, alisema Maharagande.
Hata hivyo, Maharagande alisema ushirikiano wa vyama vya upinzani, wanatarajia kufanya mkutano wa pamoja ambapo kupitia mkutano huo watatoa tamko la pamoja juu ya kamati ya madini na uteuzi wa Zitto katika kamati hiyo.
Hata hivyo, wakati viongozi wa CUF na TLP wakisema hayo, Makani ambaye pia ni mmoja wa waasisi wa Chadema alisema jana kuwa anaunga mkono uteuzi wa Zitto, lakini akasema ana wasiwasi na baadhi ya watu kuwamo katika kamati hiyo kwa kuwa walishiriki katika kuandika mikataba ya madini.
Aliwataja wanakamati hao kuwa ni pamoja na mjumbe kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na mwingine kutoka Wizara ya Nishati na Madini ambao alisema walipaswa kuwa mashahidi zaidi kuliko kuwa wanakamati.
"Kuna uwezekano wa watu hao kuitetea mikataba waliyoshiriki kuitayarisha," alisema Makani.
Hata hivyo, alisema dosari hiyo haiwezi kuwa ya msingi kiasi cha kuamua kuisusa kamati nzima kutokana na umuhimu wa madini hapa nchini.
Alisema suala la madini ambayo ni miongoni mwa rasilimali za nchi, si jambo la siasa au itikadi na kwamba, Ilani ya Chadema ilikwishaeleza mapema kwamba, mikataba ya uchimbaji madini ina matatizo na kwa sababu hiyo, ndiyo iliyomfanya Zitto aipeleke hoja hiyo bungeni kwa kuwa alikuwa anatekeleza Ilani ya chama chake.
"Alitimiza wajibu wake kama mbunge," alisema Makani.
Kutokana na hali hiyo, alisema anaunga mkono uteuzi wa mbunge huyo kwenye kamati hiyo kwa asilimia mia moja kwa kuwa utamwezesha kuwa karibu zaidi, kupambanua na kubainisha ukweli juu ya yote yatakayoshughulikiwa na kamati hiyo.
"Kufuatana na hayo, sina tatizo la uteuzi wa Zitto kwenye kamati hiyo, sina tatizo kabisa. Zitto aingie jikoni na kupakua kwa sababu anatetea maslahi ya nchi," alisema Makani na kuongeza:
"(Zitto) Akiona wanakamati wanakwenda kinyume na msimamo ambao hauna maslahi ya nchi, atakuwa huru kuandika ripoti ya kutofautiana na ripoti itakayokuwa imeandikwa na kamati.
Wengine ambao wameshatamka wazi kwamba wanamuunga mkono, Zitto kuwako katika kamati hiyo ni pamoja na mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei. Pia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amenukuliwa na vyombo vya habari vya nje, akisema yeye binafsi haoni tatizo kwa Zitto kuwako katika kamati hiyo.
Tayari Mbowe, ameitisha kikao cha Kamati Kuu ambacho kinatarajiwa kufanyika Jumamosi kujadili pamoja na mambo mengine uteuzi wa Zitto katika kamati ya kupitia upya madini.
Novemba 13, Mwaka huu, Rais Kikwete alitangaza kuundwa kwa Kamati ya kupitia mikataba na sheria za madini na kuwateua wajumbe wa kamati hiyo iliyojumuisha wajumbe kutoka kambi ya upinzani akiwemo Zitto wa Chadema na Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP) ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo.
Tangu Rais Kikwete aunde kamati hiyo na kumteua Zitto kuwa mmoja wa wajumbe wake (kamati hiyo), baadhi ya watu, wakiwamo wafuasi wa chama hicho wakiongozwa na Mbunge wa Tarime (Chadema), Chacha Wangwe, wameripotiwa na vyombo vya mawasiliano na jamii wakipinga uteuzi huo wa Zitto kwa madai kwamba, unadhoofisha hoja za wapinzani na kujenga usaliti baina yao kuhusiana na suala la madini nchini.
Kamati hiyo yenye wajumbe 12, iko chini ya uenyekiti wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu, Jaji Mark Bomani.
Wengine wanaounda kamati hiyo, ni Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Salome Makange, Kamishina wa Sera Wizara ya Fedha, Mugisha Kamugisha, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Makazi Wizara ya Ardhi, Edward Kihundwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dk Harrison Mwakyembe.
Wajumbe wengine, ni Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige, Peter Machunde kutoka Soko la Hisa, Dar es Salaam (DSE), Mkaguzi wa Mahesabu kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Mahesabu, PriceWaterHouseCoopers, David Tarimo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kodi na Mkurugenzi wa Madai na Sheria za Kimataifa, Wizara ya Katiba na Sheria, Maria Kejo.





Imeandaliwa na Muhibu Said, Elizabeth Suleyman, Salim Said na Mwanaid Omary wa MUM.


Aliyepasuliwa kichwa kwa makosa MOI sasa alishwa kwa mrija

Na Mwandishi Wetu


MGONJWA Emmanuel Didas aliyepasuliwa kichwa badala ya mguu Novemba mosi mwaka huu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) ameanza kulishwa chakula kwa kutumia mpira baada ya kushindwa kula kwa njia ya kawaida.
Hali ya mgonjwa huyo imezidi kuwa mbaya baada ya kupooza upande wa kulia na hivi sasa hawezi kula kwa njia ya kawaida badala yake anatumia mrija tangu jana usiku tofauti na alivyokuwa alipotolewa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU).
Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi jana hospitalini hapo huku wakiomba majina yao yasitajwe gazetini kwa lengo la kulinda ajira zao baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo walithibitisha kuwa mgonjwa huyo anakula kwa kutumia mpira .
�Awali tulikuwa tunamlisha kwa njia ya kawaida, lakini tangu jana tunamlisha kwa njia ya mpira hali hii inazidi kumdhoofisha kwasababu chakula anachokula kwa njia ya mpira si kingi ukilinganisha na alichokuwa anakula kwa njia ya kawaida,� alisema mmoja watumishi hao.
Ndugu wa mgonjwa aliyefika wodini hapo kwa ajili ya kumpelekea chakula alifahamisha kuwa mgonjwa huyo analishwa na wauguzi kwa njia ya mpira na kwamba hali yake imezidi kudhoofu.
Mwandishi wa habari hizi alimtafuta kaka wa mgonjwa huyo ambaye ndiye msemaji wa familia hiyo, Sists Marishay ambaye alisema kwamba hajafika hospitalini hapo tangu asubuhi hivyo hakufahamu maendeleo yake kwa leo.
�Tangu asubuhi (jana) sijaenda kumuona kwa hiyo sifahamu maendeleo yake nitakapofika huko nitakupa taarifa kamili,� alisema Marishay.
Mgonjwa mwenzake Emmanuel Mgaya aliyefanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu juzi alifanyiwa upasuaji wa kichwa ili kuondoa tatizo ambalo lilikuwa linamsumbua hali yake pia imeelezwa kuwa dhaifu tofauti na jana muda mfupi baada ya kufanyiwa upasuaji huo na amelazwa ICU akiendelea kuhudumiwa kwa karibu na madaktari wa taasisi hiyo.
Baadhi ya madaktari wanaomuhudumia walisema mabadiliko yake yanaoneka kutokana na anavyopumua kwasababu kwa sasa anapumua kwa shida tofauti na alivyo kuwa juzi baada ya kufanyiwa upasuaji huo.
Hata hivyo wasemaji wa hospitali hiyo walipotafutwa ili wazungumzie hali ya wagonjwa hao waliwakimbia waandishi kwa visingizio mbalimbali.
Afisa Uhusiano wa Taasisi hiyo, Jumaa Almasi alionekana na alipoulizwa alidai kwamba anakwenda kutafiti hali za wagonjwa hao na hakurudi tena na msaidizi wake Mary Ochieg alisemakuwa yeye si msemaji wa taasisi hiyo kisha akafunga mlango wa Ofisi yake na kuondoka.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Profesa Laurent Museru alipotafutwa ana kwa ana hakupatikana na alipopigiwa simu ili azungumzie hali ya wagonjwa hao alikata simu na kuzima kabisa baada ya kugundua kuwa anazungumza na mwandishi wa habari.
Wagonjwa hao walifanyiwa upasuaji tofauti na matatizo yao Novemba mosi, mwaka huu katika taasisi hiyo na kutokana na utata uliojitokea baada ya makosa hayo kufanyika, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo aliunda tume ya kuchunguza tukio hilo ambayo ilikamilisha kazi yake na kukabidhi ripoti yao kwa Bodi ya wadhamnini wa MOI Novemba 16, mwaka huu na Novemba 16 ikapelekwa kwa Waziri wa Afya na Ustawi ya Jamii, Profesa Devid Mwakyusa kwa hatua zaidi
.

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu