Lwakatare afungwa nje miezi 15
Lwakatare afungwa nje miezi 15
Mathias Byabato, BukobaHabariLeo; Wednesday,December 05, 2007 @00:06
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kagera imemtia hatiani Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Wilfred Lwakatare na kumfunga kifungo cha nje cha miezi 15 baada ya kupatikana na hatia ya kutishia na kufanya vurugu katika Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba . Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu wa Mahakama hiyo Wilbard Mashauri ikiwa ni takribani miezi miwili tangu Lwakatare atiwe hatiani na kufungwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa kosa la kumpiga mwandishi wa habari. Lwakatare anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 15, 2005, muda mfupi baada ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo ya jimbo hilo ambayo Lwakatare alishindwa na mgombea wa CCM Khamisi Kagasheki. Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo Faustine Fisoo dhidi ya Lwakatare aliyedai kwamba alimtishia maisha yeye, polisi na Rais wa Awamu ya Pili Benjamin Mkapa na kufanya vurugu pamoja na kutoa maneno yenye lugha chafu. Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Sheweji Alawi, aliiambia mahakama hiyo kwamba baada ya Fisoo kutangaza matokeo ya jimbo hilo kuwa ameshindwa alifika katika ofisi za halmashauri hiyo na kutoa matamshi hayo. Alidai kuwa siku hiyo Lwakatare alitamka kuwa "Nitakuonyesha cha mtema kuni au niingie msituni” hali iliyosababisha Msimamizi wa Uchaguzi kufungua mashitaka hayo. Awali katika kesi hiyo upande wa mashitaka ulileta mashahidi watano ambao wote kwa pamoja walikiri Lwakatare kutamka maneno kadhaa mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi
Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved
UJUMBE WA MHESHIMIWA RAIS
''Nyenzo Nyingine ya Mawasiliano Tanzania"
Click Here