Maisha bora hayaji kwa kubadilibadili mawaziri
Tahariri | Habari nyingine zaidi! |
Maisha bora hayaji kwa kubadilibadili mawaziri | |
Mhariri HabariLeo; Thursday,December 06, 2007 | |
KWA siku tatu sasa kumekuwa na mjadala ambao umekuwa ukiendelea katika vyombo kadhaa vya habari nchini, katika mtandao wa Intaneti na mazungumzo binafsi kuhusu matokeo ya utafiti uliofanywa na Mpango wa Utafiti na Elimu Demokrasia (Redet) wa Idara ya Sayansi ya Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuhusu utendaji kazi wa Rais Jakaya Kikwete, mawaziri, Bunge na taasisi za Serikali. Tunaheshimu matokeo ya utafiti huo, ingawa tunaelewa kwamba si lazima yawe yanaonyesha taswira kamili ya msimamo na mawazo ya Watanzania wote kwa kuzingatia idadi ndogo ya watu waliohojiwa, wilaya chache zilizohusishwa na muda mfupi wa wiki moja tu uliotumika kufanya kazi hiyo. Imani yetu ni kwamba waliobuni maswali ya utafiti huo na waliozunguka nchi nzima kuwahoji wananchi, walitumia vigezo vya kisayansi ili kuwezesha kupatikana kwa majibu ambayo yanawakilisha utashi wa Watanzania walio wengi. Matarajio yetu ni kwamba katika siku zijazo vigezo hivyo vitaboreshwa na hivyo kuwezesha kupatikana kwa matokeo yenye uhalisia zaidi. Hata hivyo, wakati tukisubiri fursa nyingine ya matokeo ya utafiti utakaofanywa na Redet au taasisi nyingine, tumeshtushwa na maudhui ya mjadala kuhusu utendaji wa Rais na Serikali na baadhi ya mapendekezo ya kutaka kufumuliwa mara moja kwa Baraza la Mawaziri kwa kutumia kigezo, kwamba wameshindwa kumsaidia Rais kutimiza kwa kasi ahadi ya kuleta maisha bora kwa Watanzania aliyoitumia wakati akiomba kura mwaka juzi. Kama ilivyoahidiwa wakati ule wa kampeni na alivyosema Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Kingunge Ngombale –Mwiru jana, suala la maisha bora ni mchakato. Hayawezi kuja kwa kufumba na kufumbua wala kunyesha kama mvua. Huo ndio ukweli ambao tunapaswa tuukubali, tuuelewe na tuuamini kwamba kinachoendelea sasa ni jitihada za dhati za kuweka mazingira yatakayowezesha kuyafikia maisha hayo kwa kasi zaidi. Inatupasa tuzingatie ukweli kuwa maisha bora hayawezi kupatikana kwa kubadilibadili mawaziri kila yanapotokea matokeo ya utafiti. |