|
---|
Makala | | OMARI NUNDU Mtanzania injinia wa ndege aliyechaguliwa bosi shirika la usafiri wa anga duniani | Ikunda Erick HabariLeo; Thursday,December 20, 2007 @00:02
| | Injinia Nundu (katikati)akiwa na wataalamu wenzake wa masuala ya usafiri wa anga. | TANZANIA inazidi kupanda chati duniani na kutambulika kama nchi mojawapo yenye wataalamu katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya usafiri wa anga.
Hivi karibuni Mtanzania, ambaye ni Mhandisi wa Ndege, Omar Nundu (59), ameweka historia nchini kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).
Nundu, ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), anakuwa mtaalamu wa pili wa masuala ya anga kutoka bara la Afrika kushika wadhifa huo.
Mwafrika wa kwanza kushika nafasi hiyo ni mhandisi wa ndege kutoka Uganda, E.Kasara, mwaka 1978.
Nundu alipata nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Desemba 14, mwaka huu, mjini Montreal, Canada.
Awali nchi za Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) zilimpendekeza Nundu agombee nafasi hiyo ya kuwa mmoja wa makamishna 19 wa Kamisheni ya ICAO.
Akielezea kuchaguliwa kwake, Ofisa Habari wa TCAA, Abel Ngapemba, anasema kwamba Mhandisi Nundu aligombea nafasi hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2005 na hakufanikiwa.
Katika uchaguzi huo wa juzi, Nundu alimshinda mpinzani wake Carlos Cirilo wa Brazil.
Nyota yake ilianza kung’ara kwenye uchaguzi wa awali uliofanyika Novemba 30, mwaka huu, katika mji huo wa Montreal, ambapo alichaguliwa kuwa mmoja wa makamishna 19 wanaoingia kwenye kamisheni hiyo, kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo. Nundu alichaguliwa kwa mara ya pili.
Kwenye kamisheni hiyo, inajumuisha wataalamu waliobobea katika sayansi ya utaalamu wa usafiri wa anga, ambao wanapendekezwa na nchi wanachama wa ICAO.
Kisha uchaguzi unafanywa na ICAO ili kupata makamishina hao 19, ambao nao wanamchagua rais wao, ambapo Nundu amepata nafasi hiyo.
Nundu ni mtaalamu wa masuala mbalimbali ya ndege katika nyanja za hesabu, usafiri wa anga, ufundi wa ndege, utungaji sera za masuala ya usafiri wa anga. Ameoa na ana watoto wanne.
Ni mwanachama wa Chama cha Wahandisi nchini tangu mwaka 1987. Pia ni mwanachama wa taasisi mbalimbali za kimataifa za Uingezera za masuala ya usafiri wa anga.
Kwenye sekta ya usafiri wa anga, kitaifa na kimataifa, Nundu ana uzoefu wa miaka 30. Awali alikuwa akifanya kazi katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATC).
Miongoni mwa kazi alizofanya katika shirika hilo ni pamoja na matengenezo ya ndege, jambo ambalo lilizidi kumjengea utaalamu zaidi.
Pia alifanya kazi katika Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAAC), Mshauri wa Masuala ya Anga wa SADC na Chuo cha Uongozi na cha Nchi za Kusini mwa Afrika (ESAMI).
Kuingia kwake kwenye kamisheni hiyo ya ICAO, kumeipandisha chati Tanzania kwa ujumla, kwa kuwa kamisheni hiyo ni muhimu sana.
ICAO ndiyo chanzo cha sheria na taratibu zote za utengenezaji ndege, viwanja vya ndege, mitambo na utaratibu wote wa kuhakikisha kwamba usafiri wa anga duniani unakuwa salama.
Wadhifa huo mkubwa duniani, unaifanya Afrika irudi kwenye historia yake baada ya miaka 60 iliyopita.
Uchaguzi wa mwaka huu, umefanya Bara la Afrika kuwa na makamishna wawili, akiwemo H. Moussa kutoka Níger na Injinia Nundu.
Katika historia ya Kamisheni ya Uongozi wa Ndege, Waafrika walioingia kwenye Kamisheni hiyo tangu mwaka 1947 ni watatu tu, ambapo wa kwanza alikuwa raia huyo wa Uganda, wa pili raia huyo wa Niger na wa tatu ni Injinia Ñundú. Ofisi ya kamisheni hiyo ipo Montreal.
Uchaguzi huo wa Nundu unaonyesha kuwa Tanzania ina wataalamu wenye sifa zinazokubalika kiushindani duniani.
Moja kati ya vitu muhimu ambavyo kamisheni hiyo inafanya ni pamoja na kutengeneza viwango vya kimataifa vyenye kulenga kuboresha usafiri wa anga na taratibu za uongozaji ndege duniani.
Wataalamu wanaoingia ndani ya Kamisheni hiyo ni lazima wawe na ushindani wa hali ya juu ili kuwashinda wataalamu wa nchi nyingine duniani zenye wataalamu kama alivyo Injinia Nundu.
Mwaka 2006 jopo la wataalamu hao 19, walimchagua kuwa Makamu wa Rais wa kamisheni hiyo, hivyo kuifanya nchi kutambulika kimataifa duniani katika nyanja ya masuala ya anga.
Waangalizi wa kimataifa wa masuala ya usafiri wa anga, wameitembelea nchi mara kadhaa kuangalia shughuli za sekta ya usafiri wa anga na kufanya ukaguzi.
Tanzania ina hati ya kuwa na anga salama kwa shughuli za usafiri duniani, jambo linaloifanya iwe na sifa kubwa kwa wawekezaji na watalii.
“Sekta ya usafiri wa anga inafanya vizuri na iko makini kuhakikisha wataalamu wenye sifa na viwango wanapatikana, ikiwa ni pamoja na kuwagharamia mafunzo zaidi wataalamu ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya mfano katika masuala ya usafiri wa anga duniani,” anasema Ngapemba.
Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved
| | | | |
|
---|
|
---|
|
---|
|
|