|
---|
Habari za Kitaifa | | Wafanyabiashara wavuna Krismasi | Waandishi Wetu HabariLeo; Tuesday,December 25, 2007 @00:02
| WAKRISTO wa Tanzania na kwingineko duniani leo wanasherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa Kristo miaka 2000 iliyopita, huku wakazi wa Dar es Salaam na sehemu kadhaa mikoani wakilalamikia kupandishwa ghafla kwa bei za bidhaa na huduma nyingine kunakodaiwa kufanywa makusudi na wafanyabiashara.
Utafiti uliofanywa na waandishi wetu, umebaini kwamba bei za bidhaa na huduma nyingi ziliongezeka bila kutarajiwa, hasa jana, na kuwafanya wawe katika wakati mgumu wa kuamua nini cha kununua au kuacha. Bidhaa kama nguo za watoto zilikuwa za gharama za juu kwa kulinganisha na siku chache tu zilizopita, kiasi cha kuwafanya wazazi na walezi wengi kushindwa kuzimudu.
Kwa upande wa usafiri wa kwenda mikoani, licha ya usimamizi mkali wa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani nauli ni za juu na baadhi ya mabasi yamejaa hadi Januari. Hata miti inayotumika kwa mapambo ya sikukuu ya leo –mikrismasi-haikupatikana wala kuuzwa kwa wingi, kwa kile ambacho wauzaji na wanunuzi walichodai kwamba ni kushuka kwa hamasa ya sikukuu.
Honest Jacob, ambaye alikuwa akiuza kiasi kidogo cha miti hiyo eneo la Forodhani, alisema waliagiza kiasi kidogo tu kutoka Lushoto baada ya kutafiti kwamba ni michache watakayoiuza. Waliyokuwa nayo jana walikuwa wakiiuza kwa Sh 10,000 na hata pungufu ilipofika jioni. Sehemu nyingine zilizozoeleka kuuzwa miti hiyo kama Tazara, Ubungo na Uwanja wa Ndege hakukuwa na ye yote aliyekuwa akiiuza.
“Yaani hata Halmashauri ya Jiji haikututoza ushuru wo wote zaidi ya kutupa kibali cha siku saba cha kuiuza hadi leo mchana na kuiacha sehemu hii safi,” alisema Jacob. Kulikuwa na pilikapilika nyingi katika mitaa, maduka na mabasi ya daladala kama ilivyokuwa katika mashine za kuchukulia fedha (ATM), ambazo zilifurika wateja hadi saa moja usiku.
Jana gazeti hili lilishuhudia maduka yakiwa yamefurika ‘watazamaji’ lakini wanunuzi wachache huku lango kuu la kuingia soko la Kariakoo jijini hapa, likionekana kuwa dogo kwa wingi wa wateja waliyokuwa wakiingia sokoni kununua na wengine wakitoka na bidhaa.
“Nimeingia na Sh 50,000 lakini nimetoka na mzigo hata kwa mkono mmoja nafika niendako. Sihitaji mtu wa kunisaidia tofauti na miaka mingine na kipindi cha kawaida,” alisikika mama mmoja aliyekuwa amebeba mfuko wa plastiki ulikuwa na bidhaa mbalimbali za vyakula. Mchele maarufu kutoka Kyela uliuzwa kwa kilo kati ya Sh 1,400 hadi 1,800 badala ya Sh 1,000 hadi 1,200 wiki iliyopita, nyama ikiuzwa hadi Sh 4,000 katika baadhi ya maeneo.
Baadhi ya wafanyabiashara walipoulizwa kwa nini wapandishe bei namna hiyo walidai kuwa kinachochangia ni kupanda kwa bei ya mafuta kunakosababisha usafirishaji wa bidhaa kuwa ghali. “Siyo kwamba ni kwa sababu ya Krismasi. Nadhani wewe pia ni mnunuzi.
Ukiangalia sana utagundua kuwa bei ya vyakula imepanda sana tofauti na miaka mingine kipindi kama hiki ni kwa sababu ya kupanda kwa mafuta katika soko la dunia, sisi ndio tunaathirika kwa kiasi kikubwa,” alisema Ludovick Kimario muuzaji wa mchele sokoni Kariakoo.
Katika mtaa maarufu wa Kongo, nguo za watoto zilizokuwa zinauzwa kwa Sh 7,000 hadi 10,000 ziliuzwa kwa Sh 14,000 hadi Sh 20,000 huku wauzaji wa vitambaa wakilalamika biashara kuwa ngumu kipindi hiki.
“Tunatamani sikukuu hizi zipite, kwani kwa upande wetu hali ni mbaya, unajua mwaka huu watu wamenunua nguo tayari zaidi special (za madukani) kuliko vitambaa. Kwa hiyo sisi tuliozoea kuuza kwa siku Sh 150,000 lakini leo (jana) na wiki iliyopita yote tunauza hata 70,000 haifiki,” alilalamika Benedict Okama, mfanyabiashara wa Mtaa wa Kongo.
Aidha, hali ni ngumu kwa wasafiri wa mikoani kwani nauli zimepanda licha ya polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa baharini na Nchi Kavu (Sumatra) kudhibiti hali hiyo, lakini tofauti na ilivyo watu wamekuwa wakinunua tiketi na kufanya baishara ya uchuuzi kwa kuwauzia wasafiri kwa bei ya juu.
Hata hivyo gazeti hili liliambiwa na wakala wa mabasi yanayofanya safari Dar es Salaam kwenda kaskazini kama Dar Express, Meridian na Scandinavia yamejaa hadi Desemba huku nauli jana zikiwa ni kati ya sh 22,000 hadi 27,000 kwa magari yote bila kujali ni Luxury au ya kawaida.
“Dada magari yote yameondoka kama unaenda limebaki hili moja na nauli ya Moshi ni sh 22,000, sema tukupe siti,” alisema wakala mmoja wa basi la Fresh Coach linalofanya safari Dar es Salaam kwenda Moshi na Arusha likiwa ni la kawaida siyo Luxury huku basi la Burudani linalokwenda Korogwe lilitoza sh 12,000 badala ya 7,000.
Kwa mujibu Sumatra mabasi yamewekewa viwango vya nauli vya aina tatu ambako Luxury kwenda mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ni Sh 25,628, Semi Luxury sh 20,860 na la kawaida sh 14,900 na yanayotokea Dar es Salaam kuelekea Tanga ni 9,600, 13,440 na 16,512 na kwenda Morogoro ni kuanzia 5,000, 7,000 na 8,600. | | | | |
|
---|
|
---|
| Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved |
|
---|
|
|