| Mshambuliaji wa timu ya Kilimanjaro Stars Erasto Nyoni (mbele) pamoja na mlinzi wa pembeni Ziriab Hussein wa Sudan wakiwa chini baada katika harakati za kugombea mpira wakati wa mchezo wa pili wa robo fainali baina ya timu hizo mbili uliochezwa jana katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam. Sudan ilishinda 2-1.(Picha na Mroki Mroki) | MATUMAINI ya Tanzania Bara kunyakua Kombe la Soka la Chalenji baada ya takriban miaka 13, yaliyeyuka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kucharazwa mabao 2-1 na Sudan katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo ya Afrika Mashariki na Kati.
Ikicheza mbele ya mashabiki waliojazana kwenye uwanja huo, Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ haikuonyesha kiwango kizuri katika kipindi cha kwanza, hali iliyowaruhusu wachezaji wa Sudan kutawala mchezo huo watakavyo.
Baada ya mechi hiyo, wachezaji wa Kili Stars wakiwa wameinamisha vichwa vyao chini walikimbia kwenye vyumba vyao ili kuepuka mashabiki wenye hasira kuwadhuru.
Kwa muda wote wa mechi hiyo, mashabiki wa soka waliokaa jukwaa kuu katika upande unaotumiwa na mashabiki wa Simba walionekana kuishangilia Sudan kwa nguvu huku wakiimba nyimbo za shangwe.
Sudan, timu pekee kutoka Afrika Mashariki na Kati, iliyofuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika zilizopangwa kufanyika mjini Accra, Ghana, Januari mwakani, ilianza kuhesabu bao la kwanza katika dakika ya 10.
Bao hilo lilifungwa na Abdelhamid Amarria kwa ufundi akiwaacha wachezaji wa Kili Stars wasijue la kufanya.
Dakika 15 baadaye, Daniel Mrwanda anayecheza soka ya kulipwa Kuwait aliisawazishia Kili Stars bao hilo baada ya kuunganisha mpira wa kona na kuujaza wavuni.
Ikiwa bado inatafakari jinsi ya kuongeza bao la pili, Kili Stars ilijikuta ikipachikwa bao jingine, mfungaji akiwa yuleyule Amarria.
Kili Stars ilibadilika kipindi cha pili na kufanya mashambulizi ya hapa na pale katika lango la wapinzani wao na kama Nizar Khalfani angekuwa makini angeweza kuisawazishia timu yake bao dakika ya 85 kwa mkwaju wa penalti.
Khalfani anayecheza soka ya kulipwa Kuwait alipiga penalti hiyo, lakini alikosa baada ya mkwaju wake kupanguliwa na kipa wa Sudan, Mohamed Adam.
Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi wa mchezo huo, Ally Kalyango wa Uganda baada ya mchezaji Vincent Barnabas kuchezewa vibaya eneo la hatari.
Akizungumza baada ya mechi, Kocha wa Kili Stars, Marcio Maximo, alisema bahati haikuwa yao kwani timu yake ilicheza vizuri hasa katika kipindi cha pili.
“Hakuna wa kumlaumu, timu nzima ilicheza na imepoteza ushindi… hiyo ni changamoto kwa wachezaji na kwa sasa najipanga kujiandaa na mechi za awali kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010,” alisema raia huyo wa Brazil.
Katika mechi nyingine ya robo fainali iliyochezwa jana, Burundi iliifunga Eritrea mabao 2-1.
Mabao ya Burundi yalifungwa na Claude Nahimana dakika ya 68 na Aime Nzohabonayo dakika ya 80 na lile la Eritrea lilifungwa na Berhane Aregaye dakika ya pili.
Kilimanjaro Stars: Ally Mustapha, Salum Sued, Erasto Nyoni, Meshack Abel, Shaaban Nditi, Mrwanda, Castory Mumbara, Michael Chuma, Uhuru Selemani, Nizar na Amiri Maftaha.
Sudan: Mohamed Adam, Ziriab Hussein, Ahmed Elbasha, Abdelhamid Amarria, Balla Gabir, Saifeldin Ali Idrisa, Nasredin Omer, Adir Bokhari Omer, Modather Eltaab, Anas Eltaher, Khalid Hassan, Akram Elhadi Salim. |