|
---|
Habari za Kitaifa | | Waziri aijia juu Dawasco | Angela Semaya HabariLeo; Sunday,December 16, 2007 @00:01
| WAZIRI wa Maji Dk. Shukuru Kawambwa amekanusha kudaiwa maji na Kampuni ya Huduma ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO) sambamba na kuishutumu mamlaka hiyo kwa kukatia maji wateja waliolipia ankara zao.
Dk. Kawambwa ametoa kauli hiyo siku chache baada ya kuandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa baadhi ya mawaziri wanadaiwa ankara za maji akiwamo yeye. Akitoa maelezo yake jana kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri alisema akiwa waziri mwenye dhamana ya kusimamia huduma ya maji hajawahi kuiba maji na Dawasco haimdai.
“Kuna habari zilidai nimeiba maji. Sidaiwi, wala sijawahi kuiba na wala sijawahi kuwa na mpango wa kuiba maji, kwa hiyo habari hizo sio za kweli,” alisema. Dk. Kawambwa alikanusha pia habari kuwa kuna mawaziri Masaki wamekatiwa maji kwa kuwa wanadaiwa na kuongeza habari hizo sio za kweli na hakuna waziri aliyewahi kukatiwa huduma ya maji.
Hata hivyo alivyoelezwa kuwa kuna baadhi ya mawaziri wamekiri kudaiwa bili za maji alisema hilo kama lipo yeye hafahamu kwani mawaziri nao ni wateja kama wateja wengine kwa hiyo Dawasco ndio inayofahamu kama mtu kalipa au hajalipa.
“Mawaziri tumepewa jukumu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, hivyo hatuwezi kufanya kinyume na hivyo…mimi nikiwa waziri mwenye dhamana ya kusimamia huduma ya maji jukumu langu kuhakikisha wananchi wanapata maji, lakini sio kujipendelea,” alisema.
Dk. Kawambwa pia aliionya Dawasco kwa kuwakatia maji wateja ambao hawana madeni na kuongeza kuwa amesikitishwa na kitendo kilichotokea wakati mamlaka hiyo ikiendesha program ya kukatia maji wateja wasiolipia ankara ambapo baadhi ya wateja walikuwa wamelipa na bado wakakatiwa maji.
“Nawataka radhi wananchi wema walioathirika na shughuli hiyo, napenda pia kusema serikali haina sera ya adhabu ya pamoja, watakaoadhibiwa ni wale ambao hawajalipia bili,” alisema. Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa ulipaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam hauridhishi hali ambayo imeshindwa kukidhi kulipia gharama za utoaji huduma hiyo na kuwataka wakazi hao kubadilika na kulipa ankara zao ili kutosheleza gharama za uendeshaji huduma itakayowafikia wananchi wengi zaidi.
Dk. Kawambwa alisema kipindi cha Julai hadi Novemba makusanyo ya Dawasco yalikuwa Sh bilioni 1.6 kwa mwezi wakati gharama halisi za utoaji huduma ni Sh bilioni 2.2 kwa mwezi jambo ambalo limesababisha serikali kubeba mzigo wa Sh milioni 600. | | | | | Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved |
---|
|
---|
| Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved |
|
---|
|
|