Monday, May 25, 2009

CCM yachukua jimbo la Busanda

Monday, 25 May 2009 11:11

(Picha) Bi Lolensia Bukwimba Mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Busanda.

Na Waandishi Wetu, Busanda

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kulitetea Jimbo la Busanda katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana na kuvunja sherehe ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokuwa kwenye mazingira mazuri ya kushinda.


Wakati CCM wakijiandaa kupokea matokeo hayo kwa shangwe na nderemo kuna habari kuwa CHADEMA wanajiandaa kuyapinga matokeo hayo.


CHADEMA ikiwa na matumaini makubwa ya kulitwaa taji hilo kutokana na mafanikio yake makubwa wakati wa kampeni kwa kujaza watu mikutanoni, matokeo hayo yamekuwa machungu kwao.

Katika kampeni hizo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alikuwa anatumia helikopta katika kampeni ambapo CCM ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Samwel Malecelea wamefanikiwa kuitungua.

Habari za matokeo hayo zinaonesha kuwa mgombea wa CCM, Lolensia Bukwimba amepata kura 29,349 akifuatiwa na mpinzani wake mkali wa CHADEMA, Finisia Magessa amepata kura 21, 249 na mgombea wa CUF, Oscar Ndalahwa kura 827 akifuatiwa na mgombea wa UDP, aliyeambulia kura 327.

Katika kinyang'anyiro hicho, CCM na CHADEMA vilichuana vikali kutokana na kuonekana kuwa vyama vyenye upinzani mkali.

CUF ambayo katika Uchaguzi Mkuu wa 2005 ilikuwa ya pili kwa mgombea wake kupata kura 26,000 imedorora na kuiachia CHADEMA kutamba ambayo mwaka 2005 ilipata kura 3,000 katika jimbo hilo.

Katika uchaguzi huo watu 133,000 walijiandikishwa kwa ajili ya kushiriki uchaguzi huo huku idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ni 52,720.

Hdi tunakwenda mitamboni viongozi wa CHADEMA, CUF na UDP walikuwa hawajafika kwenye eneo la majumlisho ya kura na waliokuwepo ni CCM peke yao.

Wakati huohuo, CUF kimepata pigo baada ya kushindwa uchaguzi mdogo wa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Magogoni. Zanzibar uliofanyika Jumamosi iliyopita.

Katika uchaguzi huo mgombea wa CCM, Asha Mohamed aliibuka mshindi kwa kura 2,474 na mgombea wa CUF, Hamad Ally Hamad alipata kura 1,974.

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu