Friday, November 30, 2007

Ukaguzi wa Benki Kuu Tanzania wabaini kasoro














Ukaguzi wa Benki Kuu Tanzania wabaini kasoro

*Ripoti za awali zaonyesha utata
*Baadhi ya vigogo BoT watajwa kuhusika
*Wahusika kuchukuliwa hatua
*Meghji asema hajaipata, iko kwa CAG
Na Ramadhan Semtawa
JOTO la tuhuma za ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) limepanda, kutokana na taarifa za awali za ukaguzi kuonyesha kuwa kuna utata katika matumizi ya akaunti hiyo.
Ukaguzi huo ulifanywa na Kampuni ya Ernst & Young katika kipindi cha siku 60, kuanzia Septemba na kukabidhi ripoti yake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wiki iliyopita.
Hata hivyo, ikiwa ni wiki moja tangu CAG kukabidhiwa ripoti hiyo, taarifa za awali kutoka vyanzo mbalimbali vya habari ndani na nje ya serikali, zinaeleza kwamba baadhi ya vigogo ndani ya BoT wanatajwa kuhusika na malipo hayo yenye utata.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, vigogo hao wanahusishwa na ama kuidhinisha au kuhusika kwa namna moja au nyingine katika malipo hayo.
Vyanzo hivyo vilifafanua kwamba, maamuzi kuhusu ripoti hiyo yanatarajiwa kuchukuliwa kabla ya mwaka mpya.
"Watu watapata zawadi ya mwaka mpya, uchambuzi unaendelea kufanyika, lakini taarifa za awali zinaonyesha hivyo," kilisema chanzo cha habari kutoka serikalini.
Vyanzo hivyo vilifafanua kwamba, kuna baadhi ya stakabadhi za malipo ambazo zimeanza kuchambuliwa na zinaonyesha kuwa zimejaa utata.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, uchambuzi huo umezingatia kwa kina nyaraka za msingi za malipo ili kuona utata huo unasababishwa na nini.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, ukaguzi huo ambao uliingia kwa ndani na kuhoji watu mbalimbali akiwemo Waziri wa Fedha, Zakia Meghji unaweza kubadili hali ya kisiasa nchini katika kipindi cha kuingia mwaka mpya wa 2007/08.
Meghji alipoulizwa ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana kuhusu ripoti hiyo, alisema hadi sasa bado iko kwa CAG.
Alisema hafahamu lolote kuhusu kilichomo ndani ya ripoti hiyo kwani hajaiona na wala hawezi kuzungumza yaliyomo kwa sasa.
"Hadi sasa ripoti iko kwa CAG, sijaipata kama ni suala la maamuzi na nini kilichomo ni hadi ichambuliwe, nikiipata, nitaipitia, atapewa Rais na maamuzi yatatangazwa kwa umma," alisema Meghji.
Kauli hiyo ya Meghji ni ya pili ambapo ya kwanza ilitolewa na CAG ambaye wiki iliyopita alisema ofisi yake inafanyia kazi mambo yaliyomo katika ripoti hiyo, lakini hakufafanua.
Ernst & Young, awali ilipaswa kuikabidhi ripoti yake serikalini Novemba 10 ikiwa ni kumalizika kwa siku 60 za kufanya ukaguzi huo, lakini haikufanya hivyo na kuiomba serikali wiki tatu kwa ajili ya kuandaa ripoti ambayo ilifanyikia London, Uingereza.
Ripoti hiyo inasubiriwa kwa hamu na Watanzania kuona ukweli wa tuhuma za ufisadi ambazo zinadaiwa kufanywa katika EPA kwa ajili ya malipo ya vocha mbalimbali.
Nchi wafadhili pia zimesema zinasubiri kwa hamu matokeo ya uchunguzi huo kwani ni kipimo cha kuona mwelekeo wao wa kuongeza misaada kwa Tanzania katika bajeti ya mwaka 2008/09.
Kampuni hiyo ilipitia mahesabu katika kumbukumbu za vocha za malipo yaliyofanywa na BoT katika kipindi cha mwaka 2005/6, kubaini kama kuna ukweli juu ya madai ya ubadhirifu wa fedha katika benki hiyo katika kipindi hicho.
Agizo la kutafuta kampuni ya kukagua vocha hizo na mahesabu ya BoT, lilitolewa na Waziri Meghji Desemba 3, mwaka jana akimtaka CAG kuteua kampuni huru ya wakaguzi wazoefu wenye sifa za kimataifa kupitia baadhi ya kumbukumbu za matumizi ya fedha za benki za mwaka 2005/2006 ili kuondoa utata.







Makala
Habari nyingine zaidi!
Alia kwa watoto wake wawili walemavu kukosa masomo



INGAWA elimu ni haki ya mtoto na msingi kwa kila mtoto, Asia Kawi na mdogo wake anaitwa Ahmed, wamekosa nafasi ya kujiunga na shule kutokana na hali yao ya ulemavu,” anasimulia mama yao Mwanahawa Juma. Mwanahawa anasema watoto wake wamekosa nafasi ya kujiunga na shule ya viziwi, jambo linalosababisha wakose elimu ambayo ingewasaidia maishani. Watoto hao wenye uchu wa elimu huamka saa 11.30 alfajiri na kuvaa sare za shule kisha kukaa sebuleni huku wakinyoosha vidole kuelekea mlango ili kuashiria kuwa wanataka kutoka nje. Wanapofunguliwa milango, watoto hukaa barazani na kuwapungia watoto wenzao wanaopita eneo hilo kuelekea shuleni. Watoto hao wanaozungumza kwa lugha ya ishara kila mara wanamsihi mama yao awapeleke shule. “Jambo hili huwa linaniumiza na ni pigo kubwa kwa watoto wangu….walizaliwa wakiwa wazima kisha wakaugua na kuteseka kipindi chote cha utoto wao…na sasa wanaendelea kuteseka kwa kukosa nafasi ya masomo,” Mwanahawa anaeleza akiwa anabubujikwa na machozi. Hivi sasa Asia ana miaka 15 lakini ameshindwa kupata elimu sahihi kulingana na ulemavu wake, kwani mama yake amejitahidi kumtafutia shule ya elimu maalumu kwa viziwi bila mafanikio. Mwanahawa anasema mtoto huyo alipotimiza umri wa kwenda shule alimpeleka katika Shule ya Msingi Viziwi Buguruni lakini hakufanikiwa kupata nafasi ya masomo. “Nilikwenda kumwandikisha katika shule ya msingi Viziwi Buguruni akajumuishwa na watoto wengine kwa ajili ya usaili na baadaye uongozi wa shule ulinijulisha kuwa amekosa nafasi,” Mwanahawa anasema kwa huzuni. Baada ya kubaini kuwa mtoto wake amekosa nafasi katika shule ya elimu maalumu kwa viziwi, aliamua kwenda kumuandikisha katika shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko. Mwanahawa alikuwa akimpeleka mwanawe shuleni kila siku kwa kipindi cha miaka minne, lakini mtoto huyo hakuwa anaelewa kitu kwa sababu hakuwa anafundishwa kwa lugha ya ishara. “Asia alichanganywa na watoto wenye taahira ya akili na mtindio wa ubongo na kuhudhuria masomo kwa miaka minne lakini alikuwa haelewi kitu chochote, hata hivyo nilibaini kuwa akifundishwa kwa lugha ya ishara anaelewa,” Mwanahawa anaeleza. Baada ya kubaini kuwa mtoto huyo anahitaji elimu maalumu kwa watoto viziwi, aliamua kutoendelea kumpeleka shule ya Uhuru Mchanganyiko kutokana na ukweli kuwa alikuwa akitembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma ambayo haipo. Anasema alirudi tena katika shule ya viziwi Buguruni kuomba nafasi kwa ajili ya Asia lakini hakufanikiwa, jambo linalosababisha mtoto huyo kukaa nyumbani. “Ahmed alipofikisha umri wa kwenda shule nilikwenda tena katika shule ya Msingi Viziwi Buguruni kuomba nafasi…walimwita kufanya usaili kisha wananiambia kuwa hakuna nafasi kwa kuwa shule hiyo inachukua wanafunzi wachache,” Mwanahawa anaeleza. Anadai kuwa ameomba nafasi hiyo kwa miaka minne mfululizo lakini hakufanikiwa, jambo linalosababisha watoto wote wawili kukaa nyumbani baada ya kukosa nafasi katika shule ya elimu maalumu kwa viziwi. Anadai baada ya kwenda katika shule hiyo mara kwa mara walimshauri ampeleke Ahmed katika shule ya Msingi Mugabe ambako kuna kitengo cha elimu maalumu kwa watoto wenye ulemavu wa kusikia na kuzungumza. Hata hivyo, Mwanahawa anasema ameshindwa kumpeleka mtoto huyo katika shule iliyopo Sinza kwa kuwa kuu mbili. Kwanza hana kipato kitakachomwezesha kugharamia nauli ya kumpeleka shule kila siku, pili ana mtoto mwingine mlemavu ambaye naye anahitaji uangalizi maalumu. “Nimetamani sana watoto wangu wasome Buguruni kwa sababu ni kama dakika saba tu kufika shuleni…ninaweza kuwashika mkono na kuwapeleka…nasikitika kwa kuwa shule ya msingi Buguruni Viziwi haipo mbali na ninakoishi, lakini watoto wangu hawakupata bahati ya kuifaidi,” Mwanahawa anasema kwa huzuni. Anaendelea kusema, “wakati mwingine nahisi kuwa umasikini wangu ndio unaosababisha watoto wangu wakose nafasi ya masomo. Kama ningekuwa na uwezo wa kifedha au cheo fulani wanangu wangepewa kipaumbele kwa kuwa ni wakazi wa Buguruni, lakini wote wawili wamekosa shule…nasikitika sana.” Mwanamke huyo mjane, asiyekuwa na uhakika kwa kupata mlo wa siku anawaomba wasamaria wema na taasisi mbalimbali zijitokeze na kusaidia kugharamia masomo ya watoto wake ili waweze kupata elimu itakayowasaidia maishani. “Bila elimu watoto hao hawataweza kushiriki vyema katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii na badala yake watakuwa mzigo…wataishi katika hali ya ufukara kwa sababu mimi mwenyewe sina uwezo wa kuwajengea msingi imara kwa maisha yao ya baadaye,” anaeleza. Katibu wa Chama cha Viziwi Tanzania, Matilda Ngonyani anasema uongozi wa shule hiyo utakuwa mstari wa mbele kujiunga na taasisi na wasamaria wema watakaojitokeza kutoa msaada kwa watoto hao. “Tumepokea kwa mshtuko taarifa kuhusu watoto hao…sisi tutawasaidia kwa kuwa kila mtoto ana haki ya kusoma kulingana na mahitaji ya ubongo wake…ikiwa kweli watafaa katika darasa la viziwi tutawapokea ingawa nafasi ni finyu,” anaema Ngonyani. Anafahamisha kuwa shule hiyo inayosimamiwa na Chama cha Viziwi Tanzania, haibagui watoto viziwi lakini inakabiliwa na changamoto kubwa kwa sababu haiwezi kuchukua wanafunzi zaidi ya 30 kwa mwaka. “Kila mwaka tunachukua wanafunzi 20 kwa darasa la kwanza na 10 wa shule ya awali…wanafunzi hao wanatoka sehemu mbalimbali nchini na tunawagharamia kila kitu…wazazi wao hawalipii chochote,” Ngonyani anasema. Hata hivyo, anasema ufinyu wa nafasi katika shule hiyo siyo sababu ya kutowapatia Asia na Ahmed nafasi ya kusoma katika shule hiyo na ameahidi kufuatilia ili kubaini tatizo. “Huenda walikosa nafasi kwa sababu wana tatizo zaidi ya moja, mfano taahiri ya akili na mtindio wa ubongo, kutokuona au ulemavu mwingine ambao unasababisha wasiendane na kundi la viziwi,” Ngonyani anaeleza. Ngonyani, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa bodi inayomiliki shule hiyo, anaeleza kuwa shule hiyo inafanya uchunguzi wa kina kuhakikisha wanaopata nafasi katika shule hiyo ni kundi la viziwi pekee ili kuepuka vikwazo vinavyosababishwa na watoto wenye ulemavu zaidi ya mmoja. “Mfano tukichukua mtoto mwenye ulemavu wa taahira ya akili na mtindio wa ubongo au mwenye otizim atakuwa anafanya mambo tofauti na wenzake hivyo watoto wengine wataacha kuzingatia masomo na kuanza kudadisi mwenendo wa mwenzao anayefanya mambo tofauti…, jambo hilo linatufanya tuwe makini sana wakati wa kuchukua wanafunzi viziwi,” Ngonyani anaeleza. Anafafanua baadhi ya watoto wenye taahira ya akili na mtindio wa ubongo au wenye otizim wana tabia ya kukaa kimya au kukaidi wanapoitwa, jambo linalosababisha wazazi waamini kuwa wana ulemavu unaosababisha washindwe kusikia na kuzungumza. Ili kubaini tatizo hilo watoto wanaopelekwa katika shule hiyo hufanyiwa uchunguzi wa masikio ili kupima uwezo wao wa kusikia. Pia hufanyiwa majaribio mengine kama vile kuchagua rangi, kupanga vitu mbalimbali kwa kufuata ukubwa na kuchora mstari. Kwa kuwa watoto hao ni wadogo tunawapa majaribio mepesi ili kutambua matatizo yao. Mfano wataalamu wanapanga herufi au maumbo yenye rangi mbalimbali ambapo mtoto anapaswa kuigizia akichagua herufi tofauti au rangi tofauti na wataalamu wanatambua ana matatizo ya macho au tatizo jingine mbali na kutosikia. “Unaweza kuchora mstari na kumuambia mtoto achore anachokiona…badala ya kuchora mstari anaandika nukta nukta au anaambiwa aweke maumbo kwenye mashimo kulingana na ukubwa anachukua umbo kubwa analazimisha liingie kwenye shimo dogo….hapo wataalamu wanabaini kuwa watoto hawa sio viziwi ila wana matatizo ya ubongo ambayo yanawakosesha mawasiliano,” Ngonyani anafafanua. Hata hivyo, anasisitiza hivi sasa Tanzania ina vitengo mbalimbali vya elimu maalumu wa watoto wenye ulemavu hivyo Asia na Ahmed hawana sababu ya kukosa elimu. “Kwa kuwa hakuna binadamu aliye kamili inawezekana hata sisi tulipitiwa…tumelichukulia suala hilo kwa uzito mkubwa …ikiwa ni viziwi tutawapatia nafasi…Asia anaweza kujiunga na shule ya ufundi na Ahmed akaingia shule ya msingi…hata wakiwa na tatizo lingine tutamshauri mama yao na kumwelekeza pa kuwapeleka,” Ngonyani anasema. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Viziwi Buguruni, Said Mkude anasema, anaomba Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza vitengo vya elimu maalumu kwa watoto wenye ulemavu ili kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata haki ya kusoma. Mkude anafahamisha kuwa amewasilisha maombi yake kwa Ofisa Elimu wilaya ya Ilala na kumfahamisha kuwa ipo haja ya kuongeza vitengo vya watoto viziwi katika shule za kawaida kwa kuwa shule yake haiwezi kuchukua watoto wote wanaomba nafasi za masomo. Akitoa mfano Mkude anasema kwa mwaka huu, watoto 78 waliombewa nafasi ya kujiunga na darasa la kwanza, kati yao wavulana 47 na wasichana 31. Waliohudhuria usaili ni 53 kati yao wavulala 33 na wasichana 20. “Kati ya wavulana 33 waliochaguliwa ni 9 na kati ya wasichana 20 waliochaguliwa ni 11 hivyo kukamilisha idadi ya wanafunzi 20 wa darasa la kwanza lenye michipuo miwili….pia tumechukua wavulana sita na wasichana wanne wa darasa la awali. Hivyo watoto zaidi ya 23 waliofanya usaili wamekosa nafasi,” Mkude anaeleza. Anaendelea kusema,"Tukijumlisha na watoto ambao hawakufika kwenye usaili ni dhahiri kuwa wastani wa watoto viziwi 45 wanakosa nafasi za masomo baada ya wazazi wao kuonyesha nia ya kuwasomesa……hivyo Serikali na wadau wa elimu wanapaswa kulipa uzito jambo hili na kulitafutia ufumbuzi ili watoto wenye ulemavu waweze kupata elimu.” Ikiwa Serikali ina dhamira ya kweli ya kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanasoma, inapaswa kufuata ushauri uliotolewa na shule vya Viziwi Bunguruni na kuongeza vitengo vya elimu maalum kwa watoto wenye ulemavu nchini. Wanaotaka kuwasaidia Asia na Ahmed wawasiliane na mama yao kwa simu namba 0754 364 085.

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu