Friday, November 16, 2007

Richard: Lazima nimrudishe mke wangu

RICHARD Bezuidenhout, ambaye ni mshindi wa shindano la Big Brother Africa II amesema changamoto kubwa analokabiliana nalo kwa sasa ni kurudiana na mkewe Ricky.
Alisema atahakikisha anaokoa ndoa yake. Richard, ambaye amejinyakulia kitita cha zaidi ya Sh milioni 130 kwa kuwa mtu wa mwisho kutoka kwenye jumba la Big Brother jijini Johannesburg, Afrika Kusini, aliwaambia waandishi wa habari kwa masikitiko kuwa moja ya changamoto zinazomkabili kwa sasa ni suala la mkewe ambaye alilazimika kurejea kwao Canada baada ya kukerwa na vitendo vya mshiriki huyo Mtanzania.
Akiwa katika jumba hilo, Richard alikuwa na uhusiano mkubwa na mshiriki toka Angola, Tatianna, uhusiano uliovuka mipaka ya urafiki wa kawaida na wawili hao kujikuta wakidondoka kwenye penzi zito na matendo yao kuonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya M-net kama ilivyo kanuni za shindano hilo.
"Kwa sasa watakaoniponda, ndio changamoto langu na hasa mke wangu ndio changamoto kubwa kwangu," alisema Richard katika mkutano na waandishi wa habari uliojaa mabishano kutokana na wenyeji wake, Multi Choice kushauri maswali juu ya maisha yake, mkewe na Tatianna yasiulizwe sana.
Hata hivyo Richard, hakuonekana kujutia kile alichokifanya wakati akiwa kwenye jumba hilo kwa siku 98 licha ya kujua kuwa alikuwa akiangaliwa na Afrika nzima, Tanzania, familia yake na mkewe Ricky kupitia kituo cha malipo cha M-Net.
"Mimi niliyeingia humo ndiye ninayejua hali ilivyo, si rahisi," alisema Richard. "Hata ingetokea kuwa narejeshwa kwenye jumba la Big Brother, ningefanya vile vile. Sio wengi ambao wanaweza kuelewa hali hiyo... mimi ndio naelewa na naweza kueleza hali inakuwaje... Yale niliyoyafanya, nilifanya kwa sababu ya mazingira ya kwenye jumba hilo.
"Lakini nasema kuwa nitajitahidi sana; nawaahidi katika mambo yatakayotokea kwa sasa ni kumrudisha mke wangu."
Akizungumzia uhusiano wake na Tatianna, Richard alisema tena kuwa ulitokana na maisha ya kwenye jumba hilo na wala si mkakati wake wa kushinda na kutwaa kitita hicho kikubwa na cha kwanza kikubwa kwa mshindani wa mashindano ya burudani kukinyakua nchini.
"Uhusiano wangu na Tatianna haukuwa mkakati wangu wa ushindi," alisema. "Kwanza sikujua kama ningekutana na Tatianna; wote tulikutana humo humo kwa hiyo isingekuwa rahisi kupanga naye.
Ushindi niliupata kutokana na jinsi nilivyo. "Mimi ni mtu huru, ni muwazi, na mtazamo wangu ni ule ule, freestyle ndio Richard... niliishi kama ninavyoishi."
Richard hakuonekana kuwa tofauti na jinsi alivyokuwa akionekana kwenye televisheni wakati wa shindano la Big Brother, lakini alifurahisha zaidi alipozungumza Kiswahili akirejea hali ilivyokuwa kwenye jumba la Big Brother.
"Kitu ambacho sikukipenda ni vile vikundi vikundi," alisema akizungumzia watu waliokuwa wakimteta.
"Wale watu walikuwa wanachonga sana; walikuwa wananiudhi sana. Walikuwa kama mademu (wanawake). Walikuwa wanaingilia sana maisha yangu; kila wakati walikuwa wanazungumzia uhusiano wangu na Tatiana, wakati wao nao walikuwa na videmu (wasichana wao) vyao.
"Tena ajabu, watu wengine walikuwa na midevu (ndevu), wana mimaso (macho), halafu eti wanakaa wananizungumzia mimi na Tatianna. Wao wana mademu zao, lakini ajabu wanakuwa wanazungumza zungumza pembeni... hata mademu zao walikuwa na wivu. Kwa kweli walikuwa wananiudhi sana."
Richard, ambaye baba wake ni chotara wa Kiholanzi na Kinyarwanda, alisema yeye ni Mtanzania halisi na si Mganda kama ambavyo imekuwa ikiandikwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo.
"Mimi si Mganda," alisema. "Mama yangu ni Mzaramo na alizaliwa hapa hapa Dar es salaam. Lakini babu yangu, yaani baba wa baba yangu ni Mholanzi na alizaa na Mnyarwanda.
Baba na mama walikutana Uganda na baada ya matatizo ya (rais aliyepinduliwa wa Uganda) Iddi Amin, waliamua kurejea nyumbani na huku ndiko nilikozaliwa."
Richard alisomea shule ya Msingi Makumbusho na baadaye kujiunga na Mashujaa kabla ya kwenda Kampala, Uganda ambako alisoma darasa la tano hadi kidato cha sita na kurejea nchini ambako sasa anasomea utengenezaji wa filamu.

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu