Sunday, December 16, 2007





Soo la Mahujaji.. JK alipigwa fiksi

Na Mwandshi wa Alasiri, Jijini

Siku moja tu baada ya Serikali kutumia `msuli` wake wa ziada katika kuwasafirisha mahujaji wote waliokwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, siri kibao zilizokuwa zimejificha kuhusiana na sakata hilo la kihistoria zimeanza kufichuka.

Vyanzo vyetu tofauti ndani ya Shirika la Ndege nchini, ATC ambalo ndio mzizi wa tukio lenyewe, Wizara ya Miundo Mbinu na kwingineko, vimeanika mambo kadhaa ambayo hapo kabla, kamwe hakuna aliyekuwa akiyafahamu.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, baadhi ya siri zilizojificha ndani ya sakata hilo lisilowahi kutokea, ni pamoja na Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, Bw. Jakaya Kikwete kupigwa changa la macho kwa kupewa matumaini yasiyokuwa ya kweli.

Yenyewe imetokea wakati dege lililokodiwa toka Afrika Kusini la MC Douglas lilipotua na mahujaji kadhaa kuruhusiwa kupanda ili waondoke, wakati ikijulikana wazi kuwa safari haipo.

Kwa mujibu wa Katibu wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzani, Sheikh Ramadhani Sanze, ni kwamba wao wanaamini Rais alipewa taarifa feki kwa sababu, mara tu baada ya yeye kuondoka zake kuelekea Marekani, mahujaji walishushwa na kuambiwa kuwa dege hilo halina kibali cha kutua Jeddah kule Saudi Arabia.

Dege kimeo
Kwa mujibu wa taarifa hizo, chanzo cha sakata lenyewe, ni kwamba dege mojawapo la ATC lililokula tenda ya kuwasafirisha mahujaji hao ni bovu.

Inaelezwa, na imethibitishwa rasmi kuwa kwa sababu hiyo, ndipo ATC ikalazimika kuingia mkataba na kampuni moja ya Saudia iitwayo Al Wasam ili isafirishe mahujaji hao. Haikusaidia, mpango mzima ukafeli.

Utapeli
Siri nyingine iliyojipambanua, ni kwamba kumbe, utapeli haupo kwenye mitaa ya wajanja huku uswazi kwetu kama Manzese, Magomeni Mapipa, Sinza na Tandika tu.

Taarifa zinadai kuwa, ATC imekutana na watoto wa mjini, waliowaingiza mkenge kwa kutotimiza hata kipengele kimoja cha makubaliano ya mkataba wao wa thamani ya mamilioni ya fedha.

ATC ikaliwa na hadi sasa inadaiwa kuwa inalia na kusaga meno kwa aibu iliyotokea!

Saundi
Inasikitisha kidogo. Kwamba, kumbe hata vibosile wenye kupiga pamba kali na tai, nao huweza kuwa mabingwa wa kupigisha watu `saundi`, bila kujali uzito wa suala lenyewe.

Mfululizo wa matukio ya kukwama kwa mahujaji unaonyesha kuwa, watu wazito katika ATC walidiriki kuwahakikishia mahujaji zaidi ya 1,000 kuwa safari yao itakuwa kama ilivyopangwa, yaani kuanzia Desemba 3 mwaka huu.

Haikuwa hivyo. Wakaahidi tena, na tena, na tena, bila mafanikio.

Mbaya zaidi, wakawaingiza hasara zaidi watu hao wanaodaiwa kulipia safari kwa dola 2,400 kwa kichwa, pale walipokuwa wakiwatajia hadi muda wa kuondoka, lakini mara kibao ikawa sivyo!

  • SOURCE: Alasiri la 15/12/2007
Posted by Picasa

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu