Sunday, November 18, 2007

Kikwete kama meli inazama tosa mizigo baharini










Kikwete kama meli inazama tosa mizigo baharini

Na Julius Magodi

KUNA simulizi moja inayoeleza adha za usafiri wa majini. Simulizi hii inamwelezea Nahodha wa meli ya Mfalme jasiri aliyetumia busara kuinusuru meli kuzama wakati ilipokumbwa na dhoruba kali ikiwa katikati ya bahari.
Meli hiyo pamoja na mizigo ya wafanyabiashara wengine ilikuwa na sanduku lililokuwa na madini na vitu vingine muhimu vya Mfalme wa nchi yake ambavyo alitoka kuvinunua nchi za mbali.
Nahodha huyo baada ya meli yake kukumbwa na dhoruba kali na kuanza kuzama aliamua kuipunguza baadhi ya mizigo kwa kuitupa baharini ili kupunguza uzito na meli isizame.
Aliwaamuru wafanyakazi wa meli hiyo kuanza kuitupa bahari mizigo hiyo, na katika harakati ya kuitupa mizigo hiyo, bahati mbaya, walitupa na lile sanduku la Mfalme.
Baada ya kupunguza mizigo meli ilirejea katika hali yake ya kawaida na baada ya muda dhoruba iliisha wakaendelea na safari yao hadi nyumbani.
Hata hivyo, mtihani mkubwa uliokuwa ukimkabili Nahodha huyo ni jinsi atakavyoeleza mpaka eleweke kwa Mfalme ambaye mizigo yake hiyo aliisubiri kwa miaka mingi mno.
Alijua hata mwelewa achalia mbali wafanyabiashara wengine waliokuwa na mizigo ambayo ameitupa baharini kunusuru meli kuzama.
Alipofika alikwenda kumwelezea Mfalme kilichotokea mpaka mizigo yake kuzama baharini. Mfalme alikasirika sana kusikia habari hiyo, lakini baada ya kutafakari sana aliona Nohodha wake alifanya jambo la busara kuitosa mizigo ili kunusuru meli kuzama.
Vile vile, hata wafanyabiashara waliokuwa mizigo yao imetupwa mabaharini ingawa walisikitika kupata hasara, nao walikubaliana na uamuzi huo kwa kujua kwamba kama meli ingezama wangekosa chombo cha kutumia kusafirisha mizigo yao.
Hatua ya Rais Jakaya Kikwete wiki hii kumteua Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kuwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya kupitia upya mikataba ya uchimbaji wa madini nchini, ninaweza kuifananisha na busara za Nahodha wa Meli ya Mfalme ya kuamua kutosa mizigo ili meli iendelee.
Nafananisha hatua hiyo na busara za nahodha wa meli, kwa sababu tangu Rais aingie madarakani miaka karibu miwili iliyopita hajaweza kuibuka kupigana na maamuzi yaliyotolewa na watu waliopo katika serikali na chama chake.
Nasema hivyo kwa sababu mara baada ya Zitto kupewa adhabu ya kusimamishwa ubunge, viongozi wa CCM walichukulia kitendo hicho kama hoja yao ya jukwaani kumlaani mbunge huyo na kueleza kuwa mambo yalikuwa shwari katika sekta ya madini.
Labda nikumbushe tu kwamba kamati ya akina Zitto itakuwa na kazi ya kuchambua mfumo wa kodi unaotumika katika sekta ya madini na kupitia mfumo wa usimamizi wa shughuli za uchimbaji mkubwa unaofanywa na serikali.
Uamuzi wa kuundwa kwa Kamati hiyo unafuatia hoja binafsi ya Zitto Kabwe aliyoitoa bungeni kutaka kuundwa kwa Kamati Teule ya kuchunguza mazingira ya kusainiwa kwa mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi nchini Uingereza na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi Februari mwaka huu pamoja na kupitiwa upya sheria ya madini kwa ujumla.
Baada ya kuwasilisha hoja hiyo, Kabwe alifungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge hadi Januari mwakani. Hatua hiyo ya Bunge iliibua mjadala mkubwa miongoni mwa makundi mbalimbali ya jamii, wakihoji sababu za kumfungia mbunge huyo kijana.
Kwa hakika, hatua ya kumteua Zitto kuingia katika kamati hiyo ni kuliambia bunge kwamba halikuwa limetenda sahihi kumfungia kijana huyo kwa hoja yake ya kutaka kuundwa kwa tume ya kuchunguza mkataba wa Buzwagi na sheria ya madini.
Pia hatua hiyo ni mwanzo wa kuanza kukataa baadhi ya maamuzi ambayo yatolewa kwa misingi ya kisiasa badala ya kuangalia maslahi ya nchi.
Uamuzi wa kumpa adhabu Zitto ulionekana kuwa jambo la kisiasa zaidi kuliko kuangalia ukweli, wabunge wa CCM ndio walionekana kuweka msimamo wa kumbana zaidi mbunge huyo.
Rais Kikwete nadhani ameichukua hatua hii akiwa anakumbuka jinsi ambavyo umaarufu wake ulivyoporomoka ghafla tangu aingie madarakani kutokana kuzingirwa na mawaziri na watendaji wengine mafisadi.
Watu walijaribu sana kumshauri Rais Kikwete mapema kwamba akitaka kufanikisha kile anachotaka kuwafanyia watanzania, basi hana budi kuvunja urafiki na watu ambao wanajiita watu bora waliokaribu naye ambao wanafanya mambo yasiyofaa kwa kivuli cha urafiki na rais.
Hata hivyo, kama anaweza bado anayo nafasi ya kurekebisha mambo yakaenda. Kuna uvumi ulioanza kuenea mitaani kutoka kwa watu wanaojiita wako karibu na rais kwamba huenda akafanya mabadiliko baraza lake la mawaziri. Kama ni kweli basi huo ni uamuzi wa busara, lakini ninachoweza kumashauri ni kwamba atose mawaziri ambao ni mizigo na sio maboya.
Atumie busara kama alizozitumia Nahodha wa Meli ya Mfalme kutosa mizigo mizito na kuacha ile mepesi inayobebeka ili meli yake iende.
Nasema hivyo kwa sababu inawezekana kabisa Kikwete akafanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri lakini akasikia uchungu kuwatupa mawaziri marafiki zake, na kuwatupa nje watendaji wazuri ili tu aonekane kafanya mabadiliko.
Kama atafanya hivyo ni wazi kwamba utawala wake utakuwa mgumu sana kutokana na kuendelea kuwa na watu katika timu yake wasiokuwa na msaada, badala yake watazidi kumharibia.
Mwandishi wa safu hii ni mhariri wa habari maalum. Anapatikana kupitia baruapepe; juliusmagodi@yahoo.com. 0754 304336
Tuma maoni kwa Mhariri

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu