Tuesday, March 4, 2008

Jumuia ya Ulaya yaibania Tanzania



Waiga mbwembwe za askari wa Bush mahakamani

na Hassan Issa, Mtwara


WAKATI wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Arusha wiki iliyopita walishuhudia vituko vya ulinzi kutokana na ziara ya Rais wa Marekani, George W. Bush, wenzao wa Mtwara mwishoni mwa wiki walishuhudia vituko kama hivyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara.

Katika kile kinachoonyesha kama ni kuiga vituo vya makachero wa Kimarekani wakati wa ziara ya Bush, askari wa Jeshi la Polisi waliopangwa kuweka ulinzi katika mahakama hiyo iliyokuwa ikisikiliza kesi ya wizi wa mamilioni ya fedha za Exim Bank, walionekana wakirandaranda huku wakiwa wamebeba silaha nzito, na kutoa amri za mara kwa mara kwa wasikilizaji wachache waliofika mahakamani hapo.

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao walikuwa wamevaa mavazi rasmi, huku wakiwa wamebeba visanduku vinavyoaminika kuwa vilikuwa na mabomu ya machozi, walitapakaa njia zote kuu za kuingilia mahakamani hapo na wengine walikuwa wamesimama kila mlango wa ofisi za mahakama hiyo.

Askari wasio na sare nao walijaa katika ukumbi wa mahakama hiyo, huku wengine wakiwa wamejichanganya na wananchi katika eneo maalum lililotengwa nje ya mahakama hiyo, huku wakiwapa amri ya kutotembea ovyo katika eneo hilo sanjari na kuwazuia wasiingie ndani kusikiliza kesi hiyo.

Askari mmoja ambaye alivalia nguo za kiraia huku akiwa na silaha begani, alikuwa kivutio kama si kituko kwa mikogo yake ya namna alivyokuwa akiichezea silaha hiyo kwa kuihamisha bega moja kwenda jingine, kuiweka kifuani na wakati mwingine kufanya kama vile anaikoki tayari kwa kuifyatua.

Waandishi wa habari waliofika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo, ambayo ni kivutio kikubwa kwa wakazi wa Mtwara, nao walionja suluba za askari hao pale baadhi ya askari walipowaita na kuwahoji na kuwaruhusu kuingia mahakamani kabla ya askari wengine kuwasimamisha kwa lengo la kutaka kuwazuia kuingia, lakini baadaye alitokea askari mwingine ambaye aliwaruhusu kuingia na kusikiliza kesi hiyo.

Kitendo hicho kilimlazimu Wakili Mwandamizi wa Serikali, Obadia Kamea, aliyekuwa anaendesha kesi, kutoa maelekezo kwa askari hao kuwa wasikilizaji waruhusiwe kuingia kusikiliza kesi na waandishi wa habari watengewe eneo lao ili waweze kufanya kazi zao bila bughudha yoyote.

Awali, mwendesha mashitaka huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa, watuhumiwa hao 10, akiwemo aliyekuwa meneja na mhasibu wa benki ya Exim tawi la Mtwara, walihusika katika wizi wa zaidi ya sh milioni 400 uliotokea Julai 24, 2004 mjini hapa.

Kamea aliwataja watuhumiwa hao waliofikishwa mbele ya hakimu Mohamed Gwae wa mahakama hiyo kuwa ni Slivester Hillu aliyekuwa meneja, Stephen Mwambene aliyekuwa mhasibu. Wengine ni Fadhili Mrapia, Abdallah Mangale, Omary Nnko, Abdulrahiman Kasimu, PC Conrad Mwingira, PC Oswald Ngonyani, Ally Siga, na PC Clement Nnko.


h.sep

Posted by Picasa

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.comme google-site-verification=Qm-XNfnL5kai8WV2inT1RRX2WIPaBTG_WPq3kYSBwbgKennedy Kimaro 2008 NYUMBANI NI NYUMBANI TU KUMBUKA KUWEKEZA NYUMBANI LEO

Rudi TOP-Juu